• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
Ramsey apata hifadhi mpya katika klabu ya Nice nchini Ufaransa baada ya kutemwa na Juventus

Ramsey apata hifadhi mpya katika klabu ya Nice nchini Ufaransa baada ya kutemwa na Juventus

Na MASHIRIKA

KIUNGO mzoefu wa Wales, Aaron Ramsey, 31, amejiunga na klabu ya Nice ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) bila ada yoyote.

Sogora huyo alisalia bila klabu baada ya Juventus kutamatisha mkataba wake nao mnamo Julai 2022 na akaanza kuhusishwa na uwezekano mkubwa wa kurejea Ramsey katika klabu zake za zamani – Cardiff City na Nottingham Forest.

Anapata hifadhi mpya katika Ligue 1 miezi michache kabla ya fainali za Kombe la Dunia kufanyika nchini Qatar kati ya Novemba na Disemba 2022. Anakuwa mwanasoka wa pili raia wa Wales kuwahi kusajiliwa na kikosi cha Ufaransa baada ya Joe Rodon aliyejiunga na Rennes kwa mkopo muhula huu.

Ramsey alijiunga na Juventus bila ada yoyote mnamo 2019 huku akidumishwa kwa mshahara wa Sh57 milioni kwa wiki.

Licha ya kusaidia Juventus kuzoa taji la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na Coppa Italia katika misimu yake miwili ya kwanza jijini Turin, Ramsey alishindwa kutamba nchini Italia jinsi ilivyotarajiwa na mashabiki.

Wingi wa visa vya majeraha ulimshuhudia akiwajibikia Juventus mara 70 katika kipindi cha misimu miwili na nusu huku akifunga mabao sita pekee.

Alichezea Juventus mara tano pekee mnamo 2021-22 na akatumia nusu ya pili ya msimu huo kuchezea Rangers ya Ligi Kuu ya Scotland kwa mkopo. Alipoteza penalti katika fainali ya Europa League iliyoshuhudia Rangers wakizidiwa maarifa na Eintracht Frankfurt ya Ujerumani.

Kwa pamoja na Federico Chiesa, Mattia de Sciglio, Kaio Jorge, Arthur Melo, Marko Pjaca na Adrien Rabiot Ramsey hakujumuishwa na kocha Massimiliano Allegri katika kikosi kilichoshiriki mechi za kujifua kwa msimu mpya wa 2022-23.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Uchaguzi mkuu sio mzaha, tujitokeze kwa...

Hofu uhaba wa unga ukiibuka kote

T L