• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:50 AM
Rhonex Kipruto kuwa kizibo cha nyota Geoffrey Kamworor mbio za mita 10,000 Olimpiki

Rhonex Kipruto kuwa kizibo cha nyota Geoffrey Kamworor mbio za mita 10,000 Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

RHONEX Kipruto amethibitishwa kuwa kizibo cha nyota Geoffrey Kamworor kwenye timu ya Olimpiki ya Kenya itakayoshiriki mbio za mita 10,000 wanaume jijini Tokyo, Japan.

Meneja wa timu ya Kenya, Barnaba Korir aliambia vyombo vya habari hapo Julai 25 kuwa mshindi huyo wa nishani ya shaba kwenye Riadha za Dunia 2019 tayari ameingia kambini katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi.

“Tunafurahia kutangaza kuwa Rhonex Kipruto ndiye mwanamichezo wa hivi punde kujumuishwa katika timu yetu ya riadha ya Olimpiki za Tokyo. Kipruto amechukua nafasi ya Geoffrey Kamworor katika mbio za mita 10,000 baada ya Kamworor kujiondoa kwa sababu ya kupata jeraha akifanya mazoezi. Tayari Kipruto ameripoti katika hoteli ya Kasarani Stadion ambako wachezaji wengine wa Team Kenya waliobaki wanaishi,” alisema Korir.

Uamuzi huo, Korir alieleza, ulifikiwa baada ya Shirikisho la Riadha Kenya (AK) kupata ruhusa kutoka kwa Kitengo cha Maadili cha Shirikisho la Riadha Duniani (AIU) ambacho ripoti yake ilionyesha kuwa Kipruto hajavunja sheria zinazopiga marufuku matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

“Rhonex ameanza kufanyiwa vipimo vya lazima vya virusi vya Covid-19 inavyohitajika kabla ya kusafiri. Mambo yakiwa sawa, atasafiri Jumatatu kuungana na wenzake Rodgers Kwemoi na Weldon Kipkirui jijini Tokyo kabla ya mbio zenyewe za mita 10,000 kufanyika Ijumaa (Julai 30),” alisema Korir.

Aidha, nyota Beatrice Chepkoech, Hyvin Kiyeng, Purity Kirui (mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji), Emmanuel Korir (mita 400 na mita 800), Ferguson Rotich na Michael Loturoomom (mita 800) waliratibiwa kuelekea Tokyo hapo Julai 25.

You can share this post!

Wanawake saba wakamatwa kwa kutengeneza pombe haramu kwenye...

Naomi Osaka aingia raundi ya tatu ya tenisi ya mchezaji...