• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
Rovanpera atoa onyo kali katika mpasho Safari Rally ikianza leo Alhamisi

Rovanpera atoa onyo kali katika mpasho Safari Rally ikianza leo Alhamisi

NA GEOFFREY ANENE

RAIA wa Finland Kalle Rovanpera alituma onyo la mapema kwa madereva wenzake kabla ya mashindano ya Safari Rally kuanza rasmi leo Alhamisi baada ya kuandikisha kasi bora katika mkondo wa majaribio (Shakedown) katika hifadhi ya Ndulele, Jumatano.

Akishirikiana na mwelekezi Jonne Halttunen katika gari aina ya Toyota GR Yaris R1, kinda huyo mwenye umri wa miaka 21 alikamilisha kilomita 5.40 katika barabara ya Loldia kwa muda wa dakika 3:42.1.

Muda wake ulikuwa sekunde 0.5 bora kuliko Mbelgiji Thierry Neuville wa Hyundai i20 N naye mshikilizi wa rekodi ya mataji mengi ya Mbio za Magari Duniani (WRC) Sebastien Loeb kutoka Ufaransa (Ford Puma) na Ott Tanak kutoka Estonia (Hyundai i20 N) wakiandikisha 3:43.9 mtawalia.

Bingwa mtetezi Sebastien Ogier, ambaye anajivunia mataji manane ya dunia, alifunga mduara wa madereva walioandikisha muda wa tano-bora. Mfaransa huyo wa timu ya Toyota GR Yaris R1, alikamilisha umbali huo kwa muda wa dakika 3:44.3.

Mkenya

Mkenya aliyekuwa na muda bora katika Shakedown ni Jeremy Wahome. Akipaisha gari la Ford Fiesta R3 na kwa ushirikiano na mwelekezi wake Victor Okundi. Jeremy alikamilisha mpasho huo katika nafasi ya 18 kwa dakika 5:06.0 akifuatiwa na Mkenya mwenzake Hamza Anwar/Adnan Din katika gari sawa na hilo kwa dakika 5:14.2.

Mkondo wa Shakedown ni sawa na wa kujipasha moto. Hufanyika katika barabara ambazo zinapeana hali halisi ya barabara za mashindano yenyewe. Loldia ilikuwa na kona nyingi pamoja na vumbi, ingawa wataalamu wa hali ya hewa wametabiri kuwa mvua itanyesha katika eneobunge la Naivasha katika kaunti ya Nakuru ambako mashindano yatafanyika.

Iwapo mvua itanyaesha, barabara zinatarajiwa kuwa na matope mengi na telezi.

“Inaonekana mwaka huu Safari Rally itakuwa ngumu hata kuliko makala yaliyopita,” alisema Rovanpera.

Katika Shakedown ya mwaka wa 2021, Ogier ndiye aliongoza kwa muda bora akifuatiwa na Elfyn Evans (Wales), Neuville (Ubelgiji), Dani Sordo (Uhispania) na Katsuta Takamoto (Japan).

Rovanpera aliambulia nafasi ya nane katika Shakedown wakati huo. Hapo jana, madereva walisafiri hadi Nairobi baada ya Shakedown magari yao yakibebwa kwa malori.

Mashindano yataanza rasmi leo nje ya jumba la mikutano la KICC. Mkondo wa kwanza wa mashindano utakuwa katika kituo cha michezo cha Kasarani utakaojumuisha kilomita 4.84. Madereva wapatao 30 watawania ubingwa katika jumla ya kilomita 363.44.

Safari Rally hii ni ya duru ya sita ya WRC baada ya Rallye Monte-Carlo (Januari 20-23), Rally Sweden (Februari 24-27), Croatia Rally (Aprili 21-24), Rally de Portugal (Mei 19-22) na Rally Italia Sardegna (Juni 2-5).

  • Tags

You can share this post!

Novartis yawekeza Sh30 bilioni kukomesha malaria na...

NDIVYO SIVYO: Ulinganifu wa hali hasi katika methali za...

T L