• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Sadio Mane asaidia Bayern Munich kukung’uta Union Berlin katika mechi ya Bundesliga

Sadio Mane asaidia Bayern Munich kukung’uta Union Berlin katika mechi ya Bundesliga

Na MASHIRIKA

SADIO Mane alirejea ugani Jumapili baada ya kupona jeraha la mguu lililomweka nje ya fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar na kusaidia waajiri wake Bayern Munich kucharaza Union Berlin 3-0 na kurudi kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Nyota huyo raia wa Senegal alijaza nafasi ya Kingsley Coman aliyechangia bao la kwanza ambalo Bayern walifungiwa na Eric Maxim Choupo-Moting na 31. Coman alipachika wavuni bao la pili la waajiri wake kunako dakika ya 40 kabla ya Jamal Musiala kufunga la tatu.

Musiala ambaye ni mfungaji bora wa Bayern kufikia sasa msimu huu, alifikisha umri wa miaka 20 mnamo Februari 26, 2023 na bao lake lilikuwa zao la krosi aliyopokezwa na kigogo Thomas Muller.

Bayern sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la Bundesliga kwa alama 46 ila kwa wingi wa mabao kuliko nambari mbili Borussia Dortmund ambao pia wametandaza mechi 22. Union Berlin ni wa tatu jedwalini kwa pointi 43, moja pekee kuliko RB Leipzig wanaofunga mduara wa nne-bora.

Union walianza mechi wakijivunia alama sawa na Bayern huku wakijivunia pia rekodi ya kutoshindwa katika pambano lolote tangu Novemba 13, 2022. Hata hivyo, walionekana kuzidiwa maarifa na Bayern katika kila idara na hawakuelekezea wenyeji wao kombora lolote.

Bayern walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya Borussia Dortmund kuwaduwaza kwa kichapo cha 3-2 katika mchuano wa awali wa Bundesliga.

Mechi kati ya Bayern na Union ilikuwa ya kwanza kwa Mane kunogesha tangu Novemba 8, 2022. Nusura afunge bao katika sekunde zake za kwanza uwanjani huku akishirikiana vilivyo na Muller pamoja na Alphonso Davies kumwajibisha kipa Frederik Ronnow.

Matokeo ya mechi hiyo yaliendeleza rekodi nzuri ya kutopigwa kwa Bayern katika uwanja wao wa nyumbani wa Allianz Arena katika mechi 18.

Awali, Dortmund walikuwa wamerejea kileleni mwa jedwali la Bundesliga kwa muda mfupi baada ya kupepeta Hoffenheim 1-0 katika ushindi uliokuwa wao wa saba mfululizo ligini.

Sasa ni pengo la alama nne ambalo linatenganisha Bayern na RB Leipzig waliokung’uta Eintracht Frankfurt 2-1 na kuwaruka SC Freiburg ambao waliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Bayer Leverkusen.

Bayern watavaana na wanyonge Stuttgart mnamo Machi 4, 2023 siku nne kabla ya kualika Paris Saint-Germain (PSG) kwa mkondo wa pili ya hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Bayern walipepeta PSG 1-0 katika mkondo wa kwanza wa kipute hicho ugani Parc des Princes, Ufaransa.

MATOKEO YA BUNDESLIGA (Jumapili);

Bayern 3-0 Union Berlin

SC Freiburg 1-1 Bayer Leverkusen

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Celtic wakomoa Rangers 2-0 na kutawazwa mabingwa wa League...

CHARLES WASONGA: Ruto, Gachagua wainue raia badala ya...

T L