• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 8:55 PM
CHARLES WASONGA: Ruto, Gachagua wainue raia badala ya kujibizana na Raila

CHARLES WASONGA: Ruto, Gachagua wainue raia badala ya kujibizana na Raila

SIDHANI kuwa gharama ya maisha itashuka hivi karibuni alivyobashiri juzi Rais William Ruto hata wakulima wakipanda na kuvuna mahindi mwaka huu.

Hali itaendelea kuwa mbaya nchini kutokana na athari za mabadiliko ya tabia-nchi, kupanda kwa bei ya kawi, kuendelea kudorora kwa thamani ya Shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni, miongoni mwa sababu nyingine.

Hii ndiyo maana serikali ya Rais Ruto inapaswa kuweka mikakati bora ya kupambana na hali hii ili kutoa afueni kwa Wakenya badala ya kutumia muda na nguvu nyingi kulaumu upinzani.

Juzi, Rais alidai kuwa kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga ndiye aliyechangia kupanda kwa gharama ya maisha kupitia handisheki kati yake na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9, 2018.

Akiongea alipoongoza hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha gesi cha Taifa katika Eneo Maalum la Kiuchumi la Dongo Kundu, Mombasa, Dkt Ruto alisema Bw Odinga hafai kuishinikiza serikali yake kushusha gharama ya maisha “ilhali ni yeye aliyesababisha matatizo katika muda wa miaka mitano chini ya serikali ya handisheki”.

Kwa kutoa kauli kama hii, Rais Ruto anaonekana kuwahadaa Wakenya.

Ninakumbuka kwamba mwaka 2022, kwenye mahojiano ya kwanza na Shirika la Habari la Al Jazeera, Oktoba 6, 2022, Rais aliungama kwamba ukame na vita vinavyoendelea nchini Ukraine ndizo sababu kuu zilizochangia kupanda kwa gharama ya maisha.

Vita vinavyoendelea Ukraine kufuatia uvamizi wa Urusi vilikatiza shughuli za usafirishaji wa mazao kama vile mahindi, ngano na mafuta ya kupikia, miongoni mwa bidhaa nyinginezo ambazo Kenya huagiza kutoka mataifa hayo mawili.

Kwa upande mwingine, ukame ambao ulianza kushuhudiwa nchini katikati mwa mwaka jana ulisababisha kuharibika kwa mahindi na mazao mengine ya chakula yakiwa mashambani.

Hali hii ilichangia wakulima kupata mavuno duni zaidi msimu uliopita. Hii ndiyo maana wakati huu kuna uhaba mkubwa wa mahindi nchini, hali inayochangia kupanda kwa bei ya zao hilo hadi kufikia Sh5,600 kwa gunia moja la kilo 90.

Ndiposa bei ya unga wa mahindi ingali juu kwani inauzwa kwa bei ya wastani ya Sh200 kwa paketi moja ya kilo mbili katika maduka mengi nchini.

Na habari mbaya hata zaidi ni kwamba wataalamu wa hali ya anga wanatabiri kwamba hali ya ukame itaendelea kushuhudiwa nchini hadi mwisho wa Mei.

Ni katika mwezi kama huu ambapo msimu wa mvua nyingi hufika kilele na wakulima huwa wamekwisha kupanda mahindi na mimea mingine ya chakula.

Haya yanajiri wakati ambapo idadi ya Wakenya wanaohitaji chakula kwa dharura inapanda kutoka watu milioni 3.5 miliomi mwaka 2022 hadi milioni 6 mwezi wa Februari 2022.

Bei ya mafuta nayo inatarajiwa kuendelea kupanda baada ya Urusi kutangaza kuwa itapunguza uzalishaji wa mafuta kutoka visima vyake kuanzia Machi.

Kwa hivyo, badala ya Rais Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua kutumia muda mwingi kujibizana na viongozi wa upinzani, wanafaa kuendeleza sera na mipango itakayowezesha Kenya kujikwamua kutoka katika hali hii.

Kwa mfano, wakomeshe ubadhirifu unaoshuhudiwa serikalini wakati huu na waelekeze pesa nyingi katika miradi ya utengenezaji mabwawa makubwa na visima ili kupatikane maji ya kuendeshea kilimo cha unyunyiziaji.

Aidha, serikali kuu na zile za kaunti ziwalipe jumla ya Sh600 bilioni zinazodaiwa na wafanyabiashara walioziuzia bidhaa na hudumu kwa mkopo pamoja na wanakandarasi waliotekeleza miradi mbalimbali na hawajalipwa.

  • Tags

You can share this post!

Sadio Mane asaidia Bayern Munich kukung’uta Union...

Midomo miwili ya serikali ya Ruto

T L