• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Sociedad wazima kabisa matumaini finyu ya Real Madrid kuhifadhi taji la La Liga msimu huu

Sociedad wazima kabisa matumaini finyu ya Real Madrid kuhifadhi taji la La Liga msimu huu

Na MASHIRIKA

MATUMAINI finyu ya Real Madrid kuhifadhi taji la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu yalizimwa kabisa na Real Sociedad kwa kichapo cha 2-0 mnamo Jumanne usiku ugani Anoeta.

Baada ya kutoshana nguvu kwa sare tasa katika kipindi cha kwanza, Real walijipata nyuma mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya Takefusa Kubo kuchuma nafuu kutokana na kosa la Eder Militao aliyekuwa akijaribu kurejesha mpira kwa kipa Thibaut Courtois.

Masaibu ya Real yalizidi katika dakika ya 61 baada ya Dani Carvajal kufurushwa ugani kwa kadi nyekundu kufuatia kadi mbili za manjano.

Sociedad waliotegemea pakubwa ubunifu wa kiungo mzoefu, David Silva, walishambulia zaidi lango la wageni wao na wakafunga goli la pili kupitia kwa Ander Barrenetxea.

Kichapo hicho kilisaza Real katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la La Liga kwa alama 68 huku pengo la pointi 14 likitamalaki kati yao na viongozi Barcelona waliokomoa Osasuna 1-0 uwanjani Camp Nou.

Real waliokuwa bila huduma za wanasoka Karim Benzema, Vinicius Junior, Luka Modric na David Alaba, walishuka dimbani dhidi ya nambari wa nne Sociedad wakiwa na ulazima wa kushinda ili kuendeleza presha kwa Barcelona.

Wakati uo huo, kuteremshwa ngazi kwa Elche kwenye kipute cha La Liga kulithibitishwa Jumanne baada ya kupokezwa kichapo cha 2-1 na Almeria ugenini. Almeria walifunga mabao yao kupitia kwa Leo Baptistao na Adri Embarba kabla ya Elche kufutiwa machozi na Ezequiel Ponce mwishoni mwa kipindi cha pili.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

PSG wamsimamisha Lionel Messi kazi kwa muda wa wiki mbili...

Mafuriko: Wakazi wa Mukuru walazimika kutumia daraja kabla...

T L