• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 7:55 AM
SS Assad FC yapania kuweka historia ya kuwa timu ya kwanza Kwale kufuzu Ligi Kuu

SS Assad FC yapania kuweka historia ya kuwa timu ya kwanza Kwale kufuzu Ligi Kuu

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KAMA kuna timu iliyowakosha wapenzi wa kandanda wa jimbo la Pwani msimu uliomalizika, timu hiyo ni SS Assad FC ambayo iliongeza idadi ya timu zinazoshiriki kwenye Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL).

Timu hiyo ya Assad iliyoko mjini Ukunda, Kaunti ya Kwale iliwashangaza mno wapenzi wa soka ambao hawakuwa na mategemeo yoyote ya kufanya vizuri kwenye Ligi ya Kitaifa Daraja la Kwanza ambapo ilifanikiwa kumaliza katika nafasi ya pili.

Meneja wa timu hiyo, Hamisi Dele aliambia Taifa Leo kuwa msimu uliopita, walipania kuhakikisha kama si ushindi basi wawe ni wenye kufuzu kupanda ngazi hadi Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) na walifanikiwa kwa lengo lao hilo.

“Ninaamini kama tulivyotia nia ya kuhakikisha tunapanda ngazi, tumetia nia kama hiyo ya kujitahidi kupanda ngazi hadi Ligi Kuu ya FKF. Lakini kwa kuwa ni mara ya kwanza kushiriki ligi hii ya NSL, tutafanya bidii kama si kushinda, basi tumalize katika nafasi nzuri,” akasema Dele.

Ili kuimarisha kikosi chake kutokana na kuwa ligi iliyoko wakati huu ni ngumu, Dele amesema wamesajili wanasoka watano kutoka timu mbalimbali.

“Tumesajili wachezaji watano kwa sababu tunataka kukiimarisha kikosi chetu kifanye vizuri,” akasema meneja huyo.

Wachezaji wao wapya waliowasajili ni aliyekuwa golikipa wa Bandari FC Omar Abdalla, Ali Juma Mwazizi kutoka Fortune Sacco FC, Shaaban Mwachozi aliyekuwa na Coast Stima (sasa Coastal Heroes) na wawili ambao hawakuwa na klabu, Omar Marere na Juma Tsala.

Wachezaji wa kikosi cha timu hiyo ya msimu huu ni Abdalla Juma (nahodha), Ali Kesi, Shaib de Gea, Joakim Daily, Juma Mwajao, Abdalla Hindo, Suleiman Ahmed, Sunday Mwaila, Abdalla Hamad Mdeka na Zakaria Mwakisu.

Wengine ni Ali Juma, Salim Dele, Rama Salim, Salim Zaire, Mathias Matabu, Briton Kitemwa, Matano Nuh Tele, Sadik Mwachotea, Ali Mwazizi, Hemedi Mwatsingwa, Heri Said, Idd Said, John Ebong na Ridhwan Mohamed.

Pambano baina ya SS Assad na Green Marine katika uwanja wa Shamu mjini Ukunda. Assad ilipata ushindi wa mabao 4-1. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Kocha Ali Marumu anasema ingawa hawakupata muda wa kutosha wa kujitayarisha kutokana na kumaliza mechi za Ligi ya Kitaifa ya Daraja ya Kwanza kuchelewa.

“Ninajua vijana wangu hawakupata muda wa kutosha wa kupumzika, lakini watafanya juhudi kutamba,” akasema Marumu.

Naye kocha wa magolikipa Hatibu Chabindo ambaye aliwahi kushikilia wadhifa kama huo katika klabu ya Bandari baada ya kustaafu kuwa kipa wa timu hiyo ya Ligi Kuu anasema magolikipa wake wako sawa na watafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanafanya vizuri.

“Nina imani kwa mafunzo niliyowapa, wameweza kunionyesha kuwa watafanya liwezekanalo kuhakikisha hata wakifungwa lakini mabao yatakuwa machache,” akasema Chabindo.

Nalo Shirikisho la Soka Nchini (FKF) tawi la Kaunti ya Kwale limeahidi kushirikiana kikamilifu na maafisa wa Assad kuhakikisha klabu hiyo inapata udhamini ili isiwe na matatizo ikiwemo gharama za ushiriki katika ligi hiyo.

Mwenyekiti wa FKF Kwale, Hamisi Mwakoja amesema watajitahidi na kushirikiana na maafisa wa Assad katika harakati za kuitafutia klabu hiyo udhamini ili wachezaji wapate kucheza soka ya hali ya juu kupigania kupanda ngazi hadi Ligi Kuu ya Kenya.

“Ninaamini kwa ushirikiano wetu na wakuu wa klabu tunaweza kufanikiwa kuipatia timu yetu hiyo udhamini ambao utaisaidia isipate tatizo la kusafiri ama gharama nyingine muhimu kwa timu ya NSL kuwa nayo,” akasema Mwakoja.

Katibu wa tawi hilo, Shilingi Fumbwe pamoja na mwakilishi wa soka ya wanawake Fatma Mwinyi walisema wana hamu kubwa ya Assad kufanikiwa kuweka historia ya kuwa timu ya kwanza ya Kaunti ya Kwale kufuzu kushiriki ligi kuu.

You can share this post!

FUNGUKA: ‘Hapa ni mahaba niue!!!’

UMBEA: Kama kweli mnapendana, hakuna kosa lisilosameheka

T L