• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
STAA WA SPOTI: Spidi yake kali ilimtoa katika voliboli na raga

STAA WA SPOTI: Spidi yake kali ilimtoa katika voliboli na raga

NA GEOFFREY ANENE

KABLA ya 2021, Ferdinand Omanyala hakuwa anajulikana kitaifa.

Hata hivyo, Omanyala sasa ni jina kubwa sio tu hapa nchini bali kote duniani.

Mwanafunzi huyo wa Digrii ya Sayansi na Kemia katika Chuo Kikuu cha Nairobi ametoka mbali hadi kufika kuwa mshikilizi wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100 – ya sekunde 9.77.

Omanyala alianza kutimka riadha mwaka wa 2016. Alipata rekodi hiyo ya Afrika baada ya kukamilisha mashindano ya Kip Keino Classic katika nafasi ya pili kwa sekunde 9.77.

Alikuwa nyuma ya Mwamerika Trayvon Bromell (9.76) katika mashindano hayo ya kimataifa yaliyoandaliwa ugani Kasarani, mnamo Septemba 18, 2021.

Omanyala alifuta ile ya awali ya raia wa Afrika Kusini, Akani Simbine (9.84).

Kasi hiyo ilimfanya kuwa wa nane-bora duniani nyuma ya Wajamaica Usain Bolt (9.58), Yohan Blake (9.69) na Asafa Powell (9.72); na Waamerika Tyson Gay (9.69), Justin Gatlin (9.74), Christian Coleman (9.76) na Bromell (9.76).

Omanyala alicheza voliboli akiwa shule za msingi za Faith Academy Ndalu na St Erastus Preparatory Naitiri katika Kaunti ya Bungoma. Kisha akaingilia raga akisoma Shule ya Upili ya Friends School Kamusinga.

“Kilichonifanya niingilie riadha ni kwamba nilikuwa winga mzuri sana kwenye raga. Mchezaji mwenzangu alinidokezea kwamba spidi yangu ilikuwa nzuri sana hivyo nijaribu riadha,” alitanguliza mshindi huyo wa tuzo ya 2021 ya mwanamichezo bora nchini Kenya, maarufu kama SOYA, kwa upande wa wanaume.

Omanyala hakushinda mashindano yake ya kwanza.

Lakini alikamilisha umbali huo kwa muda wa kuridhisha wa sekunde 10.9 kwenye duru ya Mumias ya AK mnamo Februari 2016.Anakiri safari yake ya uanariadha imekuwa na mabonde na milima.

“Changamoto zimekuwa nyingi. Kwa mfano, kupata ada ya uwanja na chumba cha mazoezi, kunyooshwa misuli, na pia majeraha. Lakini Mungu amekuwa nami wakati wote. Mchezo huu unahitaji mtu kujitolea sana,” anasema Omanyala ambaye majuzi alifanywa kuwa balozi wa Shirika la Aids Healthcare Foundation (AHF) wa chanjo ya Covid-19.

Aliwahi kupata pigo Septemba 2017 alipopigwa marufuku miezi 14 kwa matumizi ya dawa za kusisimua misuli. Alijinyanyua kutoka pigo hilo na sasa ni mmoja wa wanariadha wanaoinuka kuwa masupastaa.

You can share this post!

Waliofuja pesa NSSF wapatikana na hatia ya ulaghai wa Sh1.4...

Selina wa vishale anatamba kote nchini

T L