• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
Strathmore ni wafalme Christie 7s huku Shujaa wakiangukia pua London

Strathmore ni wafalme Christie 7s huku Shujaa wakiangukia pua London

NA GEOFFREY ANENE

STRATHMORE Leos jana Jumapili ilifanikiwa kulipiza kisasi dhidi ya KCB baada ya kuipiga 25-10 katika fainali ya shindano la kitaifa la Christie Sevens huku Kenya Shujaa ikiambulia nafasi ya mwisho London Sevens, nchini Uingereza.

Philemon Olang alifungua ukurasa wa pointi alipotinga mguso kabla ya Strathmore kufungua mwanya wa 10-0 baada ya Barnabas Owuor kuongeza wa pili.

Geoffrey Okwach alipachika mguso wa kwanza wa KCB kufanya mambo kuwa 10-5 kabla ya Mathew Mogaya kuweka Strathmore kifua mbele 15-5.

Levi Amunga alikata uongozi wa Strathmore hadi 15-10 kabla ya wanafunzi hao kutoka Chuo Kikuu cha Strathmore kuongeza miguso mingine miwili bila jibu na kuibuka washindi.

Menengai Oilers ilizaba Western Bulls 12-7 kukamata nafasi ya tatu. Strathmore ilikutana na wanabenki wa KCB katika fainali ya duru ya kwanza ya Kabeberi wiki moja iliyopita na kupoteza 12-10.

Ni taji lao la kwanza kabisa la Christie ambayo ilikuwa katika makala ya 55.

Aidha, Kenya Shujaa kwa duru ya tatu mfululizo kwenye Raga za Dunia 2021-2022 ilivuta mkia baada ya London Sevens kufika tamati ugani Twickenham.

Shujaa ilipoteza dhidi Ufaransa 31-0 katika robo-fainali ya kuorodheshwa nambari tisa hadi 16 kabla ya kulemewa na Japan 24-5 katika nusu-fainali ya kuwania nafasi ya 13-16 na kuishia kuambulia alama moja mkiani.

Vijana wa kocha Damian McGrath wana jumla ya alama 39 baada ya duru nane za kwanza za Dubai I (pointi 10), Duba II (12), Malaga (moja), Seville (nane), Singapore (tano), Vancouver (moja), Toulouse (moja) na London (moja).

Ikisalia duru moja pekee (Los Angeles Sevens mnamo Agosti 27-28), Shujaa italazimika kujikakamua zaidi kuzima wapinzani walio chini yake wakiwemo Canada, Wales na Japan wanaowakaribia kwa haraka.

Timu mbili zitakazokamilisha duru zote tisa katika nafasi mbili za mwisho zitapoteza nafasi zao kwenye ligi hiyo ambayo Kenya imeshiriki tangu msimu 2002-2003.

  • Tags

You can share this post!

Sonko atumia mbinu za kale kupenya Mombasa

Chepng’etich ang’aria wapinzani mbio za 1500m Eugene...

T L