• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Sonko atumia mbinu za kale kupenya Mombasa

Sonko atumia mbinu za kale kupenya Mombasa

NA FARHIYA HUSSEIN

ALIYEKUWA gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, amesisitiza ataendelea kutumia mbinu zake za tangu zamani kupiga kampeni za ugavana Mombasa hata anapolaumiwa na wapinzani wake.

Mwanasiasa huyo ambaye aliwahi pia kuwa Mbunge wa Makadara, Kaunti ya Nairobi mwaka wa 2010, amekuwa akishambuliwa kwa maneno na wapinzani wanaomlaumu wakidai anapumbaza wapigakura Mombasa kwa kuwapa vya bwerere.

Bw Sonko ambaye anawania ugavana Mombasa kupitia Chama cha Wiper alisema utoaji misaada kwa jamii ni njia yake ya kuwasaidia wakazi wa Mombasa kutokana na nyakati ngumu za kiuchumi.

“Wanasema kazi yetu ni kutoa fedha na kuhonga wananchi. Nchini Kenya, idadi ya watu maskini ni wengi ikilinganishwa na matajiri. Ikiwa kusaidia maskini ni makosa, nitaendelea kufanya hivyo, simwogopi mtu yeyote. Wakitaka kunipeleka jela wanaweza kufanya hivyo, walio gerezani pia ni binadamu na si wanyama. Nani alisema ninaogopa?”alisema.

Hata hivyo, mbinu hiyo ya Bw Sonko kutoa misaada kwa jamii kupitia kwa kikosi chake cha Sonko Rescue Team si jambo jipya miongoni mwa wanasiasa wengi Mombasa na Pwani kwa jumla.

Uchunguzi wa Taifa Leo umebainisha kuwa, idadi kubwa ya wanasiasa huwa wameunda wakfu ambazo wao hutumia kutoa misaada kwa umma mara kwa mara.

Mbali na wanasiasa, kampuni nyingi katika eneo hilo hutenga kiasi kikubwa cha fedha kutoa misaada kwa umma kama vile ya matibabu, usambazaji maji na vyakula miongoni mwa mengine.

Licha ya kujitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania urithi wa kiti cha Gavana Hassan Joho, mwanasiasa huyo anakumbwa na vizingiti kwani azimio lake limepingwa na wapigakura na mashirika mbalimbali mahakamani.

Anawania kiti hicho dhidi ya Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir (ODM), aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar (UDA), na Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi (PAA).

Majaji waliamua kesi dhidi ya Bw Sonko zipelekwe kwa Jaji Mkuu Martha Koome, ili aunde jopo la majaji litakalosikiliza na kuamua iwapo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inastahili kumwidhinisha kuwania ugavana.

Pingamizi dhidi yake ni kutokana na kuwa alibanduliwa mamlakani Nairobi baada ya bunge la kaunti na seneti kumpata na hatia ya ukiukaji wa sheria za maadili ya uongozi wa umma.

Hivi majuzi, alianza kummiminia sifa mgombea mwenza wake, Bw Ali Mbogo, ambaye ni Mbunge wa Kisauni, huku akisema endapo yeye atazuiwa kuwania basi Bw Mbogo ndiye anastahili kupewa nafasi hiyo ya ugavana Mombasa.

“Hizo kesi mahakamani hazitatuzuia. Tutafanya kampeni usiku na mchana kuhakikisha tunashinda kiti hicho. Hakuna kitakachonizuia,” Bw Sonko alisema.

Hivi majuzi, kura ya maoni iliyodhaminiwa na Nation Media Group ilionyesha Bw Nassir na Bw Sonko wameachana na asilimia saba pekee kwa umaarufu. Bw Sonko alikuwa na umaarufu wa asilimia 33 huku Bw Nassir akiwa na asilimia 40.

Wiki iliyopita, Bw Sonko aliandamwa na kesi nyingine ambapo mwanamke amedai amemtelekeza mtoto waliyempata pamoja.

Katika kesi hiyo iliyowasilishwa mahakamani Nairobi, mwanamke huyo anataka uamuzi utolewe ili mwanasiasa huyo awe akimlipa Sh450,000 kila mwezi kugharimia mahitaji ya mtoto anayedai ni wake.

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo kuwasilisha karatasi za uteuzi wa urais siku moja...

Strathmore ni wafalme Christie 7s huku Shujaa wakiangukia...

T L