• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Thika Queens sasa yamilikiwa na Police FC

Thika Queens sasa yamilikiwa na Police FC

NA TOTO AREGE

TIMU ya Police FC ya Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka nchini (FKF-PL) Kenya Police FC, imeanza kukuza soka ya wanawake nchini kwa kuinunua klabu ya Thika Queens.

Katika msimu wa 2022/23 uliokamilika, Thika ambao ni mabingwa mara tatu walimaliza katika nafasi ya tano wakiwa na pointi 35 kwenye msimamo wa ligi.

Akizungumza na Taifa Spoti, Chris Oguso ambaye ni Msimamizi wa idara ya Polisi ya Kenya na afisa mkuu mtendaji wa Police FC alithibitisha kuwa, klabu hiyo sasa inamilikiwa na Police FC.

“Wachezaji hawa watasimamiwa na mimi mwenyewe, Mwenyekiti wetu Munga Nyale, Makamu Mwenyekiti Bishop Akama na baraza la wadhamini. Tunataka kubadilisha picha ya timu zetu za wanawake. Tunataka kuleta weledi katika soka ya wanawake nchini,” alisema Oguso.

“Klabu itahama kutoka Thika hadi Niarobi na itabadilisha jina na kuitwa Kenya Police Bullets FC. Timu hiyo itakuwa chini ya usimamizi mpya. Tutaajiri kocha mpya, tutaajiri wachezaji wa kulipwa wengine tutawachilia na wote watakaosalia tutawapa kandarasi,” aliongeza Oguso.

Wachezaji hao pia watachukuliwa kujiunga na idara ya polisi kama wenzao wa kiume. Hili litasaidia kujiandaa kwa maisha yao baada ya kustaafu soka.

Lengo la Police kuinunua Thika ni kuambatana na sheria na kanuni za Shirikisho  la Soka Afrika (CAF).

Mnamo Septemba 2022, CAF iliweka wazi kwa wanachama wake kwamba ili timu zishiriki mashindano ya CAF zinapaswa kuwa na timu za wanawake.

“Haswa kwa vigezo vya michezo vilivyopo kwenye Kanuni za Leseni za Klabu za Wanaume za CAF (toleo la 2022). CAF sasa imeleta sharti kwa timu za soka za wanaume. Klabu ambazo zinatarajia kushiriki mashindano ya CAF  lazima ziwe na angalau timu moja (01) ya wanawake. Timu hiyo lazima pia iwe inayoshiriki katika shindano lililoidhinishwa na chama cha wanachama,” ujumbe huo wa CAF ulisema.

Kwa sasa, Ulinzi Stars ndiyo timu pekee inayoshiriki FKF-PL ambayo ina timu ya wanawake inayojulikana kama Ulinzi Starlets.

Katika Ligi Kuu ya Kitaifa (NSL), Vihiga United wana Vihiga Queens, huku Kisumu All Stars wakiwa na timu ya Kisumu All Starlets.

  • Tags

You can share this post!

Nahodha John McGinn kuendelea kuchezea Aston Villa hadi 2027

Waislamu waunga mchakato wa serikali kulainisha makundi ya...

T L