• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 5:55 AM
Ufaransa, Ubelgiji mizanini Euro 2024

Ufaransa, Ubelgiji mizanini Euro 2024

NA MASHIRIKA

PARIS, Ufaransa

WAFARANSA wataalika Waholanzi nao Wabelgiji watavaana na Waswidi kwenye menyu ya michuano mikali ya kufuzu kushiriki Kombe la Bara Ulaya (Euro) mwaka 2024, leo Ijumaa.

Mabingwa wa Kombe la Dunia 2018 Ufaransa wanafukuzia ushindi wa nne mfululizo dhidi ya Uholanzi ugani Stade de France.

Hata hivyo, mchuano huu utakuwa mtihani kwa vijana wa Didier Deschamps baada ya mshambulizi matata Karim Benzema, kipa nambari moja nahodha Hugo Lloris na nambari mbili Steve Mandanda na beki stadi Raphael Varane kustaafu kuchezea taifa.

Mabeki Wesley Fofana na William Saliba pamoja na kiungo N’Golo Kante wako nje kwa sababu ya majeraha.

Ufaransa almaarufu Les Bleus itategemea washambulizi matata Kylian Mbappe, Kingsley Coman na Antoine Griezmann na mkongwe Olivier Giroud.

Nahodha mpya Mbappe aliyefunga mabao matatu katika fainali ya Kombe la Dunia 2022 dhidi ya Argentina na atatumai kuendeleza makali hayo.

Uholanzi ina kocha mpya Ronald Koeman baada ya Louis van Gaal kustaafu. Oranje itakosa huduma za kiungo wa Barcelona, Frenkie de Jong anayeuguza jeraha.

Waholanzi hawana rekodi nzuri dhidi ya Ufaransa. Wamepoteza mechi 14, kutoka sare tatu na kushinda 11. Walipepeta Ufaransa 2-0 kupitia mabao ya Georginio Wijnaldum na Memphis Depay walipokutana mara ya mwisho Novemba 2018.

Wijnaldum, Depay na Cody Gakpo ni baadhi ya wakali wa Uholanzi.Naye, mfumaji ‘mzee kabisa’ katika Ligi Kuu ya Italia, Zlatan Ibrahimovic,41, ataongoza Uswidi dhidi ya Ubelgiji.Uswidi imepoteza mara tatu mfululizo dhidi ya Ubelgiji.

Itategemea mshambulizi Alexander Isak,23, dhidi ya Ubelgiji iliyo na nahodha mpya Kevin De Bruyne baada ya Eden Hazard kustaafu.

Pia, ‘mashetani wekundu’ wako chini ya kocha mpya Domenico Tedesco baada ya Roberto Martinez kutemwa. Poland ina kocha mpya Fernando Santos aliyeondoka Ureno baada ya miaka minane kufuatia masikitiko ya Kombe la Dunia 2022.

Santos atategemea mfumaji matata Robert Lewandowski dhidi ya Czech inayojivunia wachezaji matata kama Patrik Schick na Tomas Soucek. Czech ilizaba Poland 1-0 mara ya mwisho zilikutana 2018 mjini Gdansk na pia ilipokuwa mwenyeji 2-0 mwaka 2009. Mataifa 53 yaliyogawanywa katika makundi 10 yanawania tiketi 23 kuungana na wenyeji wa dimba la Euro 2024, Ujerumani.

  • Tags

You can share this post!

Rufaa yatupwa, magaidi 2 kukaa jela miaka 41

Teranga Lions, Atlas Lions na Super Eagles mavizioni kufuzu...

T L