• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Ushindi wa Wanjiru waipa Kenya dhahabu ya 3 Poland

Ushindi wa Wanjiru waipa Kenya dhahabu ya 3 Poland

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA mara sita wa Afrika, Grace Wanjiru ameshindia Kenya medali ya tatu ya dhahabu kwenye Riadha za Dunia za Ukumbini za watimkaji wanaozidi umri wa miaka 35 mjini Torun, Poland, Jumanne. 

Wanjiru aliachia wapinzani wenzake vumbi katika fani ya matembezi ya haraka ya mita  3,000 uwanjani Arena Torun, siku moja baada ya Erick Sikuku na Kenneth Mburu kubeba mataji ya matembezi ya haraka ya 3,000m na mbio za nyika za kilomita nane katika washiriki walio na umri kati ya miaka 45 na 49 mtawalia.

Rebecca Mulatya alinyakua nishani ya fedha ya kuruka umbali (Long Jump) siku ya Jumatatu kwa kinadada walio kati ya miaka 45 na 49.

Mnamo Jumanne, mwanaolimpiki Wanjiru hakusikitisha katika kitengo chake cha wanawake walio kati ya miaka 40 na 44 baada ya kutwaa taji kwa muda wake bora msimu huu, dakika 14 na sekunde 15.19.

Amekamilisha mbele ya Mhispania Maria Valero (14:57.97), Mwitaliano Marina Ivanova (15:52.26) na Wahispania Isabel Perez (16:24.62) na Natividad Vidal (16:39.40) waliokamata nafasi tano za kwanza. Watembeaji 15 walishiriki kitengo hicho.

Kenya inawakilishwa na wanariadha 18 katika mashindano hayo ya kila baada ya miaka miwili yaliyoanza Aprili 26.

Kwa sasa, Kenya inapatikana katika nafasi ya 20 ikiwa na dhahabu tatu na fedha moja.  Ujerumani imekaa juu ya jedwali kwa medali 95 (dhahabu 31, fedha 30 na shaba 34) ikifuatiwa na Poland (dhahabu 30, fedha 29 na shaba 18) na Amerika (dhahabu 16, fedha 18 na shaba saba).

Tunisia ni ya pili barani Afrika na 31 duniani kwa dhahabu moja, fedha moja na shaba moja.

  • Tags

You can share this post!

Haji asitisha kesi dhidi ya binti ya CAS

‘Kaunti jirani zipige jeki Coast General’

T L