• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:50 AM
Vihiga Queens kuanza dhidi ya Ulinzi Starlets msimu mpya wa 2023-24

Vihiga Queens kuanza dhidi ya Ulinzi Starlets msimu mpya wa 2023-24

NA TOTO AREGE

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Nchini (KWPL), Vihiga Queens, watafungua msimu wa 2023-24 dhidi ya wanajeshi wa Ulinzi Starlets ugani Mumias Sports Complex, Kaunti ya Kakamega hapo Septemba 23, 2023.

Timu hizo mbili zilimaliza msimu uliopita katika nafasi ya kwanza na ya tatu mtawalia.

Ulinzi, ambao pia walitetea Kombe la Wanawake la FKF, watakuwa wanapania kutwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya kwanza msimu mpya.

Wageni Ligi Kuu Kenya, Police Bullets ambao wamesajili wachezaji wazoefu, watakipiga nyumbani dhidi ya Soccer Assassins FC ugani Police Sacco jijini Nairobi.

Assassins kwa sasa wako nchini Rwanda kwa mashindano ya Afrika Mashariki ya Shule za Upili.

Gaspo Women watamenyana na Bunyore Starlets ugani Stima Club jijini Nairobi. Nakuru City Queens  watawaalia Wadadia Women katika uwanja wa Maonyesho ya Kilimo mjini Nakuru.

Kwa upande mwingine, Transa Nzoia Falcons watakuwa wenyeji wa Zetech Sparks ugani Ndura mjini Kitale.

Wakati uo huo, FKF imefanya badiliko katika ligi ya Divisheni ya Kwanza ambapo wameanzisha Ligi ya Kitaifa ya Wanawake (NSL) kama ilivyo katika ligi ya wanaume.

Timu za NSL zimechaguliwa kutoka kwa timu za FKF-WPL msimu wa 2022/23 ambazo zilishushwa daraja na timu zilizofanya Divisheni ya Kwanza msimu jana.

Ligi hiyo itagawanywa katika Zoni mbili ambayo ni A na B na itajumuisha timu kutoka mikoa ya Nairobi na Pwani. Zoni B itashirikisha timu kutoka mikoa ya Nyanza na Bonde la Ufa.

Timu ambazo zitashiriki Zoni A ni pamoja na Uweza Women (Nairobi), Mathare United Women (Nairobi), Mombasa Olympic (Pwani), MTG United (Pwani), Falling Waters Barcelona (Nairobi), Sunderland Samba ( Nairobi), Macmillan Queens (Nairobi), Kangemi Starlets (Nairobi), na Kayole Starlets (Nairobi).

Timu kutoka Nyanza ni pamoja na Kisumu All Starlets, Kisped Queens, Gideon Starlets na Kolwa Falcons pamoja na Royal Starlets, Eldoret Falcons na Gene Queens kutoka Bonde la Ufa zimepangwa Zoni B.

Kila Zoni itakuwa na jumla ya timu 10. Ligi hiyo imepangwa kuanza Septemba 30, 2023.

Ligi ya Divisheni ya Kwanza pia itagawanywa katika Zoni nne ambazo ni A,B,C na D.

Zoni A itajumuisha timu kutoka Nairobi, Mashariki mwa Kenya, huku Zoni B ikiwa na timu kutoka Pwani.

Zoni B itashirikisha timu kutoka Nyanza na Bonde la Ufa huku Zoni D ikiwa na timu kutoka Mgharibi na Bonde la Ufa. Ligi hiyo itaanza rasmi Oktoba 14, 2023.

  • Tags

You can share this post!

Nyayo House kuna maradhi ya ufisadi, akiri Kindiki

Kundi la Wabunge wa Pwani lapata viongozi wapya

T L