• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Wanariadha 40 wa Team Kenya wakita kambi Kigari kwa mbio za nyika za dunia

Wanariadha 40 wa Team Kenya wakita kambi Kigari kwa mbio za nyika za dunia

Na AYUMBA AYODI

TIMU ya taifa ya Kenya itakayoshiriki mashindano ya Mbio za Nyika za Dunia nchini Australia mwezi Februari, itakuwa na kambi ya mazoezi katika Chuo cha Walimu cha Kigari katika kaunti ya Embu.

Mshirikishi wa timu hiyo John Kimetto alifichua Alhamisi kuwa changamoto za kimipango zimewalazimu kuchagua kambi yao ya kawaida ya Kigari badala ya maeneo ya Nandi, Kericho, Uasin Gishu ama Machakos yaliyokuwa yamependekezwa.

“Mandhari, miinuko, chakula kipya na ukarimu wa chuo cha Kigari unasalia kuwa bora na hatukutaka kubadilisha mazingira hayo mara moja,” alisema Kimetto. “Hatukutaka kupata mishtuko ya mazingira mabaya ambayo ingesumbua wanariadha wanaofanya mazoezi katika maeneo mengine.”

Hata hivyo, Kimetto alisema kuwa watazuru maeneo tofauti kama Nandi mapema siku zijazo kwa lengo la kuona uwezekano wa timu kufanyia mazoezi.

Kimetto aliongeza kuwa ingawa kambi ilifunguliwa Jumatatu, wanatarajiwa kikosi kizima cha Kenya hapo Jumapili baada ya wakimbiaji kadhaa kuomba ruhusa washughulikie majukumu mengine.

Baadhi ya watimkaji ambao hawajafika kambini ni bingwa wa Jumuiya ya Madola mbio za mita 5,000 Beatrice Chebet, mshindi wa nishani ya fedha ya Jumuiya ya Madola 10,000m Daniel Simiu na mshindi wa medali ya shaba ya Riadha za Dunia za Ukumbini 1,500m Abel Kipsang. Watatu hao walifuzu kuwa polisi katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi cha Kiganjo hapo Jumanne.

Chebet alinyakua dhahabu katika makala yaliyopita ya Mbio za Nyika za Dunia mwaka 2019 mjini Aarhus, Denmark katika kitengo cha chipukizi.

Wanariadha wengine ambao hawajaingia kambini ni mshindi wa medali ya fedha ya Riadha za Nusu-Marathon Duniani Kibiwott Kandie na mshikilizi wa rekodi ya dunia mbio za 3,000m kuruka Beatrice Chepkoech.

Kenya ina kikosi cha wakimbiaji 40. Mbio hizo za dunia ni Februari 18 mjini Bathurst, Australia.

Kikosi cha Kenya: Wanaume (10km) – Sebastian Kimaru, Daniel Simiu, Kibiwott Kandie, Emmanuel Kiprop, Nicholas Kipkorior, Geoffrey Kamworor. Watimkaji wa akiba ­- Collins Koros, Hillary Kipchirchir; Wanawake (10km) – Grace Loibach, Edinah Jebitiok, Irene Cheptai, Agnes Jebet, Viola Chepng’eno, Emily Chebet, Beatrice Chebet. Mkimbiaji wa akiba – Cynthia Chepng’eno; Wanaume (8km) – Ismael Kirui, Reynold Kipkorir, Dennis Kipkirui, Raphael Dabash, Gideon Kipng’etich, Charles Rotich. Watimkaji wa akiba – Stephen Masinget, Daniel Kinyanjui; Wanawake (6km) – Faith Cherotich, Sheila Chebet, Joyline Chepkemoi, Nancy Cheriop, Marion Chepng’etich, Diana Cherotich. Wakiambiaji wa ziada – Pamela Kosgei, Diana Chepkemoi; Wanaume (2km mbio mseto) – Emmanuel Wanyonyi, Daniel Munguti, Mathew Kipsang, Abel Kipsang; Wanawake (2km mbio seto) – Brenda Chebet, Miriam Cherop, Beatrice Chepkoech. Mtimkaji wa akiba – Betty Chelangat.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Laura Rua

Mabondia Wakenya Okwiri, Wanyonyi waapa kumaliza Watanzania...

T L