• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
Xavi Hernandez arejea nyumbani Uhispania kuwatia makali masogora wa Barcelona

Xavi Hernandez arejea nyumbani Uhispania kuwatia makali masogora wa Barcelona

Na MASHIRIKA

KIUNGO wa zamani wa Barcelona, Xavi Hernandez, 41, amerejea kambini mwa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), mara hii akiwa kocha.

Mkufunzi huyo raia wa Uhispania amepokezwa mkataba wa miaka mitatu uwanjani Camp Nou baada ya kuagana rasmi na kikosi cha Al Sadd ambacho kimekuwa kikijivunia huduma zake tangu 2019.

Kwa mujibu wa Barcelona, mkataba wa Xavi utaendelea kwa muda wote uliosalia katika msimu huu wa 2021-22 na kwa mihula mingine miwili ijayo. Xavi anatarajiwa kutambulishwa rasmi kwa mashabiki, wasimamizi na wachezaji wa Barcelona hapo mnamo Novemba 8, 2021 uwanjani Camp Nou.

“Haikuwa ‘kwaherini’, ilikuwa ‘tuonane hivi karibuni’. Uwanja wa Camp Nou umekuwa nyumbani kwangu siku zote. Nyinyi ni mashabiki wangu na watu wangu. Barcelona ndiyo klabu ninayoipenda zaidi. Sasa ninarejea nyumbani. Tuonane hivi karibuni,” akatanguliza Xavi kupitia video fupi kwa mashabiki wake.

Xavi aliwahi kuongoza Uhispania kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia na mataji mawili ya soka ya bara Ulaya (Euro). Alichezea Barcelona jumla ya mechi 767 na akaongoza kikosi hicho kujitwalia mataji 25 kwa kipindi cha miaka 17 akiwa katika timu ya kwanza. Aliondoka Barcelona na kujiunga na Al Sadd mnamo 2015, akiingia katika sajili rasmi ya kikosi hicho mara ya kwanza akiwa mchezaji.

Alipokezwa mikoba ya ukocha baada ya kustaafu soka mnamo 2019 na akaongoza Al Sadd kutwaa ufalme wa Ligi Kuu ya Qatar mnamo 2020-21. Chini ya Xavi, Al Sadd hawajapoteza mechi yoyote kutokana na 36 zilizopita ligini.

Tangu Barcelona wamtimue kocha Ronold Koeman mnamo Oktoba 27, Xavi amekuwa akihusishwa pakubwa na uwezekano wa kurejea Camp Nou kuwa mrithi wake alikohudumu kwa kipindi kirefu zaidi akiwa mchezaji.

Kufikia sasa, Barcelona wanakamata nafasi ya tisa kwenye msimamo wa jedwali la La Liga baada ya kushinda mechi nne kati ya 11 za ufunguzi wa muhula huu na kujizolea pointi 17. Ni pengo la alama 10 ndilo linatamalaki kati yao na viongozi wa jedwali, Real Madrid.

Barcelona wamekabiliwa na panda-shuka tele za usimamizi na kifedha huku wakishindwa pia kurefusha kandarasi ya nyota Lionel Messi aliyehiari kuyoyomea Ufaransa kuvalia jezi za Paris Saint-Germain (PSG).

Kufikia sasa, Barcelona hawajawezeshwa kutumia fedha zozote kwa minajili ya sajili wapya huku wakijinasia huduma za wanasoka Memphis Depay, Sergio Aguero na Eric Garcia bila ada yoyote. Mvamizi Luuk de Jong alijiunga na Barcelona kwa mkopo kutoka Sevilla ambao pia ni washiriki wa La Liga.

Awali, Joan Laporta ambaye ni rais wa Barcelona alikuwa amesema: “Nimekuwa nikisema siku moja Xavi atakuwa mkufunzi mkuu wa Barcelona lakini sijui ni lini.”

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mbinu za Uhuru kuzima Ruto

Real Madrid yakung’uta Rayo Vallecano na kutua...

T L