• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Mistari ya Raila yakosa kumnasa Aisha Jumwa

Mistari ya Raila yakosa kumnasa Aisha Jumwa

VALENTINE OBARA na MAUREEN ONGALA

JUHUDI za wanasiasa wapinzani wa Naibu Rais William Ruto, kumvuta upande wao Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, zimepata pigo baada ya mbunge huyo kukataa mistari yao.

Taifa Jumapili ilibainisha kuwa awali kulikuwa na mikakati ya kutaka kumshawishi Bi Jumwa aondoke katika mrengo wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Mikakati hiyo ilikuwa inaendelezwa na wanasiasa katika Kaunti ya Kilifi ambao wanaegemea upande wa Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, chini ya muungano wa Azimio la Umoja.

Bi Jumwa, ambaye aliasi ODM na amepanga kuwania ugavana Kilifi, jana alijitokeza wazi kukana uvumi kwamba alikuwa anazingatia kumwasi Dkt Ruto.

Wawili hao wamesimama pamoja tangu Bw Odinga alipoweka mwafaka wa maelewano na Rais Uhuru Kenyatta mwaka wa 2018.

“Mimi Aisha Jumwa sitapiki kisha nikarudi nikalamba. Msimamo wangu ni thabiti ndiposa huwa napenda kutumia msemo wa mlingoti chuma, kamba chuma na bendera chuma. Siwezi kusukumwa hapa na hapa nikatikisika,” akasema, kwa video fupi aliyosambaza katika mitandao ya kijamii.

Mdahalo kuhusu uaminifu wake kwa UDA ulizidi wiki iliyopita, alipokosa kuhudhuria mikutano ya hadhara ya chama hicho katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Mikutano hiyo ilikuwa ya kwanza ya UDA kuandaa pamoja na vyama vya Amani National Congress (ANC) kinachoongozwa na Bw Musalia Mudavadi, na Ford Kenya cha Moses Wetang’ula.

Akiwa mmoja wa waakilishi wakuu wa Pwani katika kikosi cha Dkt Ruto, mbunge huyo alitarajiwa na wengi kuwa mstari wa mbele sawa na jinsi alivyokuwa katika mikutano ya awali.

Hata hivyo, inashukiwa kutohudhuria kwake kulitokana na kuwa, alikosa kuhudhuria kesi dhidi yake kuhusu madai ya kuhusika kwa mauaji, na mahakama ikaambiwa alikuwa anaugua.

“Niko ndani ya UDA kama mmoja wa waanzilishi wa chama. Mimi Aisha hakuna hata siku moja nimewahi kufikiria ama kupigwa na mshipa ati mimi naenda azimio la kuzimia. Niko imara kwa sababu nimejitolea kuwa tegemeo la watu wa Kilifi,” akasema.

Katika mahojiano ambayo Taifa Jumapili ilifanya na wafuasi mbalimbali wa Azimio la Umoja walio Kaunti ya Kilifi, ilisemekana mikutano ilifanywa kutafuta jinsi ambavyo Bi Jumwa angeshawishiwa kujiunga na muungano huo.

Mwenyekiti wa ODM tawi la Kilifi, Bw Teddy Mwambire, alithibitisha kutaka kumshawishi Bi Jumwa arudi upande wa Bw Odinga, hasa baada ya baadhi ya wanasiasa waliokuwa wameasi chama hicho awali kutangaza wataunga mkono azimio la kinara huyo kwa urais.

Alisema yuko tayari kuwapokea pia mbunge wa Kilifi Kaskazini Bw Owen Baya, na Bw Michael Kingi wa Magarini.

“Niko tayari kuwapokea wale walio katika vyama vingine na kuwapa mwongozo bora kwa sababu ni dhahiri kuwa chama cha UDA hakiendi popote na naibu wa rais William Ruto atapoteza katika uchaguzi mkuu wa Agosti. Hakuna mtu anayetaka kujihusisha na mtu atakayeanguka,” akasema.

Mmoja wa wanasiasa wanaopanga kuwania ugavana wa kaunti hiyo alifichua kuwa, Bi Jumwa alikuwa anatakiwa kushiriki katika mazungumzo ya kikundi cha wawaniaji ugavana wanaotaka kuunga mkono mmoja wao, ambao ni wa upande wa Bw Odinga.

Mwanasiasa huyo ambaye tumembana jina kwa vile hana idhini kuzungumzia masuala ya ndani ya kundi lao, alisema Bi Jumwa alikuwa tayari ameonyesha nia ya kutaka kushirikishwa kwa mazungumzo.

“Wagombea hawa wanaunga mkono wazo hili ya kwamba viongozi wakae pamoja. Kwa sasa tunasubiri siku ambayo tutakaa na kulipiga msasa jambo hilo,” akasema.

Baadhi ya wafuasi wa Chama cha Pamoja African Alliance (PAA), pia walieleza kumtaka Bi Jumwa aungane nao.

PAA ambayo inaongozwa na Gavana wa Kilifi Amason Kingi, inampigia debe Bw Odinga kwa urais.

You can share this post!

UJAUZITO NA UZAZI: Kukabiliana na matatizo wakati wa...

Uhuru aelekezea Ruto makombora

T L