• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Bunge kufanya vikao vingine vitatu kukamilisha mswada tata wa vyama vya kisiasa

Bunge kufanya vikao vingine vitatu kukamilisha mswada tata wa vyama vya kisiasa

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ameitisha vikao maalum vya bunge la kitaifa kwa siku tatu ili kukamilisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Kisiasa.

Hii ni baada ya wabunge kufeli kukamilisha shughuli hiyo katika kikao maalum kilichofanyika Jumatano, Desemba 29, 2021 na kilichokumbwa na vurugu na mapigano.

Katika tangazo lililochapishwa magazetini Ijumaa, Desemba 31, 2021 Bw Muturi alisema ameitisha vikao hivyo mnamo Januari 5, 6 na 7, 2022; siku za Jumatano, Alhamisi na Ijumaa.

“Vikao hivyo vitafanyika katika ukumbi wa Bunge la Kitaifa, Nairobi kuanzia saa nne asubuhi (10.00 am) na kuanzia saa nane na nusu mchana (2.30 pm). Wabunge watashughulikia mswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya kisiasa na shughuli nyingine ambazo zitaratibiwa,” akasema Bw Muturi.

Spika huyo pia ameamuru karani wa bunge la kitaifa Michael Sialai kuhakikisha kuwa mfumo wa upigaji kura kielektroniki unafanya kazi ili kufanikisha shughuli hiyo.

“Wabunge ambao huenda wamepoteza kadi zao za kupiga kura kielektroniki wanahitajika kuchukua kadi mpya kutoka kwa afisi ya Mlinzi Mkuu wa bunge kufikia saa kumi na moja jioni (5.00 pm) mnamo Jumanne, Januari 4, 2022,” akaongeza Bw Muturi.

Mnamo Jumatano usiku, kiongozi wa wengi Amos Kimunya alithibitisha kuwa alimwandikia barua Spika Muturi ili aitishe vikao vitatu maalum kufuatia fujo zilizotokea katika kikao cha siku hiyo.

Fujo zilizoandamana na vita kati ya wabunge wa mirengo hasimu, zilivuruga mipango ya kukamilishwa kwa mswada huo tata unaopendekeza kuundwa kwa vyama vya miungano.

“Ningependa kuchukua fursa hii kuripoti kwamba tayari nimetuma ombi kwa Mhe Spika nikitaka aitishe vikao vitatu maalum juma lijalo ili tumalize kazi hii,” akasema Bw Kimunya ambaye ni Mbunge wa Kipipiri.

Mapigano yalizuka bungeni katika kikao cha Jumatano hali iliyocheleweshwa kukamilishwa kwa hoja zilizowasilishwa na wabunge kadhaa, wengi wao wakiwa wale wa ‘Tangatanga’, waliotaka baadhi ya sehemu za mswada huo ziondolewe au zifanyiwe marekebisho zaidi.

Baadhi ya wabunge hao ambao ni wandani wa Naibu Rais William Ruto, pia walitumia mbinu ya kuibua sarakasi nyingi ambazo zilichukua muda mwingi.

Kwa mfano, wengi wao walipopewa nafasi ya kupiga kura walitumia karibu dakika 15 wakisifia chama cha United Democratic Alliance (UDA) huku wakikashifu vuguvugu la Azimio la Umoja na kiongozi wake Raila Odinga, kabla ya kupiga kura.

Vurugu zilizozuka bungeni zilichangia kujeruhiwa kwa Mbunge wa Sigowet/Soin Benard Kipsengeret Koros alijeruhiwa usoni na kiongozi wa wachache John Mbadi.

Kitendo hicho kilichangia spika wa muda Christopher Omulele kumfurusha Bw Mbadi na kumwamuru asihudhurie vikao vitano vya bungeni.

“Nimeshambuliwa katika bunge hili na jabali wa vita. Sasa siwezi kuona. Siwezi kupiga kura, Bw Spika,” akasema Bw Koros.

Vurugu hizo zilitokea wakati wa upigaji kura kuhusu hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Kandara Alice Wahome aliyetaka kuondolewa kwa sehemu ya 6 ya mswada huo inayopendekeza kuundwa kwa vyama vya muungano.

Mswada huo uliangushwa na wabunge wa mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa kura 158 dhidi ya kura 134 za wabunge wa mrengo wa ‘Tangatanga’ waliounga mkono.

  • Tags

You can share this post!

Man-United wapepeta Burnley na kurukia nafasi ya sita...

Kiungo Mejbri wa Man-United ajumuishwa katika kikosi cha...

T L