• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Man-United wapepeta Burnley na kurukia nafasi ya sita kwenye jedwali la EPL

Man-United wapepeta Burnley na kurukia nafasi ya sita kwenye jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United walifunga mabao matatu katika kipindi cha kwanza kwa mara ya kwanza tangu Januari 2021 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kukomoa Burnley 3-1 mnamo Alhamisi usiku ugani Old Trafford.

Ushindi huo wa Man-United wanaonolewa na kocha Ralf Rangnick uliwapaisha hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 31 sawa na West Ham United.

Bao la Scott McTominay katika dakika ya nane ndilo lilikuwa la haraka zaidi kwa Man-United kuwahi kufunga ligini tangu Disemba 2020 nyota huyo raia wa Scotland alipocheka na nyavu za Leeds United mwanzoni mwa kipindi cha kwanza.

Jadon Sancho alipachika wavuni bao la pili la Man-United katika dakika ya 27 kabla ya Cristiano Ronaldo aliyepoteza nafasi nyingi za wazi kukamilisha krosi ya McTominay na kumwacha hoi kipa Wayne Hennessey.

Masihara ya Eric Bailly katika ya 38 yaliwezesha Aaron Lennon kufutia Burnley machozi. Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Burnley kusakata ligini tangu Disemba 12, 2021. Kichapo kutoka kwa Man-United kiliwasaza katika nafasi ya 18 kwa alama 11 sawa na Newcastle United.

Ushindi wa Man-United uliendeleza rekodi ya kutoshindwa kwao tangu wamtimue kocha Ole Gunnar Solskjaer. Mabingwa hao mara 20 wa EPL sasa wanajiandaa kuvaana na Wolves uwanjani Old Trafford mnamo Januari 3, 2022 huku Burnley wakipangiwa kumenyana na Leeds United ugani Elland Road mnamo Januari 2, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Obure naye atangaza kugombea ugavana Kisii

Bunge kufanya vikao vingine vitatu kukamilisha mswada tata...

T L