• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
CECIL ODONGO: Wandani wa Ruto Mlima Kenya wamemgeuka?

CECIL ODONGO: Wandani wa Ruto Mlima Kenya wamemgeuka?

Na CECIL ODONGO

HUENDA sasa ni dhahiri kwamba Naibu Rais Dkt William Ruto hana hakika ya kuungwa mkono na wanasiasa wa Mlima Kenya, hasa baada ya baadhi ya wandani wake kumgeuka ghafla na kupigia kura mswada wa mpango wa Maridhiano (BBI).

Baadhi ya wabunge ambao wamekuwa wakipaza sauti majukwaani kukemea mswada huo, hasa kutoka eneo la Mlima Kenya, walishangaza kwa kuupigia kura bungeni.

Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri amekuwa kati ya wanasiasa waliokuwa wakikashifu BBI na hata kuapa katika mojawapo ya mikutano kuwa katu hawezi kuunga mkono.Wabunge wengine walioshangaza kuunga BBI japo wamekuwa mrengo wa Dkt Ruto ni Anthony Kiai wa Mukuruweini na Mary Wa Maua wa Maragua.

Bw Ngunjiri hasa amekuwa mwandani wa Dkt Ruto hasa machoni mwa jamii ya Mlima Kenya eneo la Nakuru na Bonde la Ufa kwa ujumla. Ilishangaza kuwa alipigia kura mswada huo ilhali amekuwa akiwashutumu viongozi kutoka eneo hilo walioko katika mrengo wa Kieleweke.

Kwanza, Bw Ngunjiri ambaye bado anashikilia kwamba yeye ni jemedari halisi wa Dkt Ruto, alijitetea kuwa mswada huo utaipa kaunti ya Nakuru maeneobunge matano zaidi, kuwaongezea nafasi ya uwakilishi na pia pesa za CDF.

Huenda Bw Ngunjiri ni fuko ndani ya kambi ya Naibu Rais kwa sababu inakuaje kuwa alipinga mswada huo lakini ikifika wakati wa kura anaungana na upande mwingine eti kwa maslahi ya raia?

Je, kuna hakikisho gani kuwa atapinga mswada huo kwenye kura ya maamuzi iwapo mwishowe Naibu Rais ataamua kuipinga kutokana na masuala yanayohusiana na uongozi ambayo amekuwa akiyaibua.

Hapo atayafuata maslahi ya raia au Naibu Rais ?Wandani wengine wa Dkt Ruto kutoka eneo la Kati pia walipiga kura ya kupinga mswada huo.

Je, wao hawafahamu kuwa maeneo bunge mapya yataongezwa Mlima Kenya BBI ikipita?Kwa hivyo, Bw Ngunjiri na wabunge wengine waliopigia kura mswada huo, ni wasaliti na kile kilichojitokeza miongoni mwa wafuasi wa Dkt Ruto mashinani ni kuwa hawaaminiki.

Japo, Dkt Ruto alitoa taarifa kwamba hakuwaagiza wabunge hao kuchukua msimamo maalum kuhusu BBI, hilo halina mashiko kwa kuwa tayari waliomkaidi wanaonekana kama wasaliti.

Kulingana na matukio hayo ya kisiasa huenda viongozi wengi wa Mlima Kenya wanamdanganya Naibu Rais lakini mpigo wa moyo wao uko kwingine huku wakisubiri mwelekeo kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Kura ya BBI inaelekea katika Bunge la Seneti leo na inasubiriwa kuona iwapo viongozi wanaounga mkono azma ya Dkt Ruto hasa kutoka Mlima Kenya watafuata nyayo za Bw Ngunjiri.

Kando na hayo vigogo wengine wa kisiasa wa Mlima Kenya kama Bw Mwangi Kiunjuri ambaye alikuwa akichukuliwa kuwa mwandani wa Dkt Ruto, sasa amegeuka na kuanza kujitwika jukumu la kupatanisha mirengo ya Kieleweke na Tangatanga.

Yamkini Bw Kiunjuri amegundua kuwa huenda mambo yakawa tofauti 2022 na anajiweka pazuri ili kuegemea upande ambao utakuwa salama na kuvutia raia zaidi.

You can share this post!

MARY WANGARI: Wazazi watumie likizo kuwapa watoto malezi...

Kiambu Community FC yakuza vipaji vya soka na kuhimiza...