• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
CECIL ODONGO: Yashangaza mno wazee kutawaza watu kiholela

CECIL ODONGO: Yashangaza mno wazee kutawaza watu kiholela

Na CECIL ODONGO

Hatua ya mabaraza ya wazee ya kuwatawaza na kuwaidhinisha wanasiasa wanaomezea mate kiti cha urais mwaka ujao kiholela bila kuzingatia iwapo wana uwezo wa kupigania maslahi ya raia inatia doa ushawishi wao katika jamii ya sasa.

Japo mabaraza haya zamani yaliheshimiwa na sauti zao kusikizwa na jamii, hali ni tofauti sasa huku wengi wa wakongwe hawa wakikubali kuwaidhinisha au kupigwa picha na wanasiasa kwa maslahi yao ya kibinafsi.

Mwenendo huu ni usaliti mkubwa kwa kuwa miaka mingi ya nyuma, wazee walikuwa wakitoa mwelekeo kisiasa kulingana na matakwa ya jamii kwa kukumbatia kiongozi bora tena maarufu badala ya hali ya sasa ambao uzito wa mifuko ya mwanasiasa inaonekana kuwateka.

Mnamo Jumatano, baadhi ya wazee wa jamii ya Bukusu walimuidhinisha Waziri wa zamani wa Biashara Dkt Mukhisa Kituyi kuwania kiti cha urais 2022 kwenye hafla iliyohudhuriwa na Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na Gavana wa Makueni Profesa Kivutha Kibwana.

Ingawa kuna uhuru wa kidemokrasia, kuna uwezekano finyu kuwa Dkt Kituyi anaweza kushinda kiti cha urais akilinganishwa na Moses Wetang’ula ambaye amekuwa akidhibiti siasa za kaunti za Bungoma na Trans Nzoia ambako Wabukusu ni wengi.

Hili linazua swali iwapo nia ya wazee hawa ni kumfurahisha tu mbunge huyo wa zamani wa Kimili kwa manufaa yao ya kifedha.

Pia kuidhinishwa huku kuna nia gani ilhali baadhi ya wazee wa eneo hilo wamekuwa mrengo wa Kinara wa ANC Musalia Mudavadi anayeonekana kama kiongozi ambaye yupo katika nafasi nzuri kuwawakilisha kitaifa kutokana na umaarufu wake?

Katika eneo la Ukambani, Baraza la Uongozi la Jamii hiyo ambalo linashirikisha koo 22 mnamo Julai lilimuidhinisha Profesa Kibwana kuwania urais 2022 na pia kusaka uungwaji mkono kutoka jamii nyingine.

Hii ni licha ya baraza la jamii ya Akamba hapo awali kumtawaza Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kama msemaji wa jamii hiyo na anayefaa kuingia ikulu 2022 baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu.

Kama tu Dkt Kituyi Magharibi, Profesa Kibwana hana uungwaji mkono wa maana Ukambani na hata maeneo mengine nchini. Kwa hivyo, kuwania kwake urais huenda kukazigawanya kura za jamii hiyo na kuyeyusha zaidi ushawishi wa Bw Musyoka katika siasa za kitaifa.

Vivyo, Mlimani hadi leo umegawanyika baada ya Spika Justin Muturi kutawazwa kama msemaji wa Gema Baraza la jamii ya Ameru (Njuri Ncheke) mnamo Machi pamoja na lile la Agikuyu mnamo Juni mwaka huu.

Suala hilo lilizua mgawanyiko miongoni mwa wanasiasa na wazee wa eneo hilo na ushawishi wa Bw Muturi bado haujahisiwa vyema eneo hilo.

Majuzi alipokuwa katika ziara yake eneo la Nyanza, mfanyabiashara mwanasiasa Jimi Wanjigi alimtembelea mwenyekiti wa Baraza la Wazee Waluo Willis Otondi kupokea baraka zake kwenye azma yake ya kuwania urais kupitia tiketi ya ODM.

Matukio haya ya kuidhinisha tu wanasiasa kiholela yanaonyesha tamaa ya fedha iliyokolea miongoni mwa wazee wa mabaraza ya jamii mbalimbali.Kwa hivyo, wapigakura wanafaa kutathmini ufaafu wa kiongozi yeyote badala tu ya kumpigia kura kutokana na mwelekeo uliotolewa na wazee.

You can share this post!

CHARLES WASONGA: IEBC iruhusu Wakenya wote walio ughaibuni...

Wakulima wa chai kulipwa bonasi ya juu mwaka ujao