• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Wanaume wa Kenya wajikwaa dhidi ya Nigeria voliboli ya Afrika ya ufukweni

Wanaume wa Kenya wajikwaa dhidi ya Nigeria voliboli ya Afrika ya ufukweni

Na AGNES MAKHANDIA akiwa Agadir, Morocco

TIMU ya wanaume ya voliboli ya ufukweni ya Kenya ilipata pigo katika kampeni za kufuzu kushiriki Olimpiki baada ya kupoteza dhidi ya Nigeria kwa seti 2-1 mjini Agadir, Juni 22.

Wakenya Ibrahim Oduor na James Mwaniki walikuwa wa kwanza kujibwaga kwenye changarawe dhidi ya Ezeke Emenike na Chidebere Okeke na kulimwa kwa seti 2-0 (21-16, 21-16).

Ushirikiano wa Brian Melly na Enock Mogeni ulifufua matumaini uliposawazisha 1-1 baada ya kupiga timu ya kwanza ya Nigeria ya Simion Hillary na Obayemi Ogunshina 2-0 (21-15, 21-13).

Kocha Patrick Owino aliamua kutumia Melly na Mogeni katika mechi ya tatu ya kuamua mshindi naye mwenzake kutoka Nigeria, Ajilore Kayode akatumia Okeke na Emenike. Katika mechi hiyo ya kufu-kupona, Melly na Mogeni walianza vibaya wakijipata chini alama 3-6 na 5-9, huku Nigeria ikiwaadhibu kwa kukosa kulinda safu yao ya nyuma vyema.

Emenike alikuwa mwiba kwa Wakenya hao karibu na neti aliposaidia timu yake kufungua mwanya zaidi 10-18 kabla ya vijana wa Owino kupoteza seti hiyo 13-21.

Mogeni na Melly walishirikiana vyema katika seti ya pili na kuiongoza 8-5 na 15-13. Mogeni kisha alisukumia Okeke makombora matatu mazito yaliyozalisha pointi. Kenya iliendelea kutesa Nigeria, ingawa mawasiliano mabovu na uamuzi mbaya kutoka kwa Wakenya hao wawili ulishuhudia Nigeria ikipunguza mwanya huo hadi 20-17 na 20-18 kabla ya Kenya kunyakua seti hiyo 21-19.

Seti ya tatu na mwisho ya kuamua mshindi kati ya Kenya na Nigeria ilikuwa nipe-nikupe. Timu hizo zilikuwa pointi 4-4 na 10-10, lakini uzoefu wa Wanigeria ukawasaidia kufunga kazi kwa alama 15-13.

Owino alikiri kuwa mchuano huo ulikuwa mgumu. “Lazima tuimarike katika mechi zijazo. Bado tuna matumaini na ninaamini kuwa timu zetu zitajinyanyua kabla ya kukutana na Mali hapo Jumatano,” alisema Owino.

Kayode alisema ushindi dhidi ya Kenya ulikuwa muhimu sana kwao. “Kenya ina kikosi imara na kupata ushindi dhidi yao ni onyo kali kwa wapinzani wengine. Hata hivyo, hatutapotoshwa na ushindi huu kwa sababu ngoma imeanza tu,” alisema kocha huyo wa Nigeria.

Mali pia ilianza kampeni yake vibaya kwa hivyo mchuano wa Jumatano utakuwa moto. Timu hiyo ilipoteza kwa mechi 2-0 mikononi mwa Msumbiji.

Kenya, Nigeria, Msumbiji na Mali ziko Kundi B. Kundi A linaleta pamoja Morocco, Tunisia na Sudan. Ghana, Afrika Kusini, Misri na Congo Brazzaville zinaunda Kundi C. Kundi D linajumuisha Gambia, Rwanda, Togo na DR Congo.

TAFSIRI NA GEOFFREY ANENE

You can share this post!

Google taabani kwa kupendelea teknolojia yake katika...

Echesa alikuwa amemletea Ruto Wazungu wawili alipokamatwa,...