• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Fataki zalipuka mdahalo wa ugavana ‘001’

Fataki zalipuka mdahalo wa ugavana ‘001’

NA WINNIE ATIENO

WAWANIAJI kiti cha ugavana katika Kaunti ya Mombasa kupitia vyama vya Usawa kwa Wote, Pamoja African Alliance (PAA) na United Democratic Alliance (UDA) Jumamosi walielezea nia ya kufufua uchumi wa Kaunti ya Mombasa.

Ili kuimarisha uchumi wa kaunti hiyo, wawaniaji hao walieleza kuwa wataishinikiza serikali kuu irejeshe huduma za Bandari katika jiji la Mombasa, iwapo watachaguliwa katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Abdulswammad Nassir wa chama cha ODM, Daniel Munga (mgombea huru), Awiti Bollo wa Vibrant Democratic Party, ni miongoni mwa waliokosa kuhudhuria mdahalo huo uliosheheni masuala ya bandari.

Kuhamishwa kwa Bandari ya Mombasa hadi Nairobi na Naivasha, kulichangia biashara nyingi Mombasa kufungwa na mamia ya vijana kukosa ajira.

Hata hivyo, wagombea wa ugavana walilitumia suala hilo kusaka kura, wakiapa kurejesha huduma hiyo Mombasa ili watengeneze nafasi za kazi.

Wawaniaji wa kiti hicho wakiongozwa na Naibu Gavana wa Mombasa, Bw William Kingi (PAA), aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar (UDA) na Bw Said Abdalla (Usawa Kwa Wote), waliapa kuhakikisha wakazi wamenufaika na rasilimali yao ya bandari.

Wakiongea kwenye mdahalo wa ugavana wa kaunti hiyo, walimlaumu Gavana Hassan Joho kwa uongozi mbaya uliopelekea uchumi wa Mombasa kuzorota.

“SGR iliua uchumi wa Mombasa. Nikichaguliwa nitahakikisha operesheni za bandari zimerejeshwa ili watu wetu wapate ajira. Isitoshe, nitawapa wawekezaji mazingira bora ili wawekeze Mombasa na kufungua nafasi za kazi,” alisema Bw Abdalla.

Bw Omar alisema kuwa, baada tu ya kuapishwa kwa mpeperusha bendera ya urais wa mrengo wa Kenya Kwanza Naibu wa Rais, Dkt William Ruto kama rais, atahakikisha huduma ya bandari imerejeshwa Mombasa.

Haya yanajiri baada ya wakazi wa Mombasa kuweka mkataba na Bw Ruto, kurejesha rasilimali hiyo ili wenyeji wanufaike.

Bw Omar alimlaumu Gavana Joho akisema kuwa alifaidi pakubwa na biashara ya uchukuzi baada ya huduma ya bandari kuhamishwa.

“Gavana Joho ana kandarasi ya kuhamisha mizigo kutoka SGR Mombasa hadi Nairobi. Yaani mtetezi amekuwa mnyonyaji. Mgombea wetu wa urais William Ruto atakapoingia serikalini atafutilia mbali kandarasi hizo,” alisema Bw Omar.

“Tutapanua ajira na kufufua uchumi kupitia huduma za bandari. Kadhalika, tutawapa wafanyabiashara wadogo wadogo pesa, ili waendeleze biashara zao. Katika afya tutajenga hospitali, kununua vifaa vya kuboresha sekta hiyo mbali na kuajiri wafanyakazi zaidi,” akasema.

Alisema atawekeza kwenye usafishaji wa maji ya bahari kwa kutumia teknolojia maalumna kuongeza kuwa atafanya hivyo kukabiliana na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo adimu jijini Mombasa.

Bw Omar alihoji kuwa, atakabiliana na swala tata la unyakuzi wa ardhi na uskwota.

“Tutahakikisha wanyakuzi wa ardhi za serikali wanafuatwa na ardhi hizo kurejeshewa wenyewe. Pia nitaweka sheria ya kusimamisha ubomoaji wa kiholelaholela,” alisema.

Dkt Kingi, ambaye uhusiano wake na Bw Joho umeanza kusambaratika, baada ya kudai kuwa alipokonywa gari lake rasmi hivi majuzi, alidai kuwa wakazi wa Mombasa hawanufaiki na bandari, ambayo ni rasilimali yao.

Hata hivyo, alisema atashirikiana na serikali kuu kuhakikisha Mombasa inanufaika na rasilimali hiyo, iwapo atachaguliwa Agosti 9. Pia alisema atawaweka kwenye mstari wa mbele vijana, walemavu na kina mama, hasa biashara zao.

“Watachukua mikopo kutoka kwa hazina maalum ya kaunti, ambayo tutaitenga kwa ajili yao. Serikali kuu haikutuhusisha ilipohamisha biashara zote za bandari hadi Naivasha na Nairobi. Hii ndio sababu ya uchumi wetu kudorora,” alisema Dkt Kingi.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Heri ahadi chache zitimiazo, kuliko rundo la hewa

Joho asihi wanasiasa wa Mombasa kuungana ‘kwa manufaa...

T L