• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
TAHARIRI: Heri ahadi chache zitimiazo, kuliko rundo la hewa

TAHARIRI: Heri ahadi chache zitimiazo, kuliko rundo la hewa

NA MHARIRI

MSIMU wa ahadi ndio sasa unapamba moto huku wawaniaji kila pande wakitafuta mbinu kushawishi wapiga kura.

Takriban kila mwaniaji sasa hivi, kuanzia kwa urais hadi kwa udiwani amesheheni ahadi.

Juzi, Muungano wa Azimio wa Raila Odinga ulizindua manifesto yao na ilikuwa na ahadi nyingi zilizohusu kuimarisha uchumi, kubuni nafasi za kazi na kulinda waliotengwa katika jamii.

Ni Manifesto ambayo wachanganuzi wanasema, mengi bado yatategemea vigezo vingine ambavyo haviwezi kuthibitishwa kwa sasa.

Kimsingi, waliweka upatikanaji fedha za kufadhili ahadi hizo katika kuzima ufisadi ili kukusanya mabilioni yanayoporwa. Lakini hilo litategemea na mambo mengi ambayo hayawezi kutathminiwa kwa sasa.

Naibu Rais William Ruto naye Ijumaa akaandaa kongamano la wanawake ambapo alitia saini makubaliano ya kutekeleza ahadi kemkem kwa wanawake. Ikabainika pia kwamba ahadi hizo zitahitaji kitita kikubwa cha pesa kuzifanikisha, jambo linaloibua maswali kuhusu nia kamili ya wanasiasa kutoa ahadi.

Je, wana lazima gani kubwabwaja mambo mengi ambayo hata kwa mtoto wa umri wa miaka minne atakwambia kwamba ni ndoto? Haswa haya yakijiri nyuma ya pazia ya ahadi za serikali ya Jubilee ambayo iliingia hatamuni kwa matao ya juu na ahadi zilizometameta ilhali ikaishia kufanya machache pekee huku idadi kubwa ingali ikilalamikia maisha yao kurudi nyuma katika utawala wao?

Mbona wanasiasa wasitoe ahadi chache lakini ziaminikazo?

You can share this post!

UJAUZITO NA UZAZI: Minyoo wanaohangaisha watoto

Fataki zalipuka mdahalo wa ugavana ‘001’

T L