• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 2:54 PM
Gachagua aahidi kupiga marufuku mchele wa nje

Gachagua aahidi kupiga marufuku mchele wa nje

NA GEORGE MUNENE

MGOMBEA mwenza wa urais katika Kenya Kwanza Rigathi Gachagua, Ijumaa aliendesha kampeni katika kaunti ya Kirinyaga akiahidi kupiga marufuku mchele kutoka nje ili kulinda wakulima wa mpunga eneo hilo.

Alisema mchele unaoagizwa kutoka ng’ambo hutoa ushindani kwa ule unaozalishwa eneo hilo na kuathiri mapato ya wakulima.

Huku akionekana kumshambulia Rais Uhuru Kenyatta, Bw Gachagua, aliilaumu serikali ya Jubilee kwa kuruhusu mchele wa bei rahisi kuingizwa nchini.

“Wakulima hawawezi kupata faida kwa sababu wanunuzi wengi huishia kununua mchele wa bei rahisi kutoka Pakistan. Serikali ya Kenya Kwanza italinda wakulima kwa kupiga marufuku mchele unaoingizwa nchini kutoka nje ili wakulima wetu wapate faida,” akasema alipohutubu katika kijiji cha Rukanga.

Bw Gachagua alilalamika kuwa wakulima wa Mwea ambao huzalisha asilimia 80 ya mchele unaotumiwa nchini wamekuwa wakipata hasara kwa kukosa usaidizi kutoka kwa serikali.

“Serikali inafahamu fika kwamba wakulima wanateseka ilhali inaendelea kuruhusu kuingizwa kwa mchele wa bei rahisi kutoka nje. Serikali ya Dkt William Ruto haitakubali hali kama hii kuendelea,” mbunge huyo wa Mathira akasema.

Aliwataka wakulima wa mpunga kujiandaa kuzalisha mchele kwa wingi ili wapate faida kubwa kutokana na jasho lao pindi Dkt Ruto atakapochukua hatamu za uongozi wa nchi hii.

“Vile vile, tutauza mchele kwa wanajeshi na taasisi nyingine za serikali ili wakulima wapate faida kubwa,” Gachagua akakariri.

Aidha, aliongeza kuwa serikali ya Dkt Ruto itaanza mpango wa kuwafidia wakulima endapo mazao yao yataharibika ili wasipate hasara.

Bw Gachagua alitoa wito kwa wakazi kujitokeza kwa wingi na kumpigia kura Dkt Ruto ili wapate faida kutokana na mchele wao.

“Ili wakulima wajikomboe kutoka kwa unyanyasaji wanafaa kumpigia Dkt Ruto kura,” akaongeza.

Bw Gachagua vile vile, aliisuta serikali kwa kuwalipa maafisa wa polisi mshahara duni ambao hufanya kazi kubwa kulinda maisha ya Wakenya na mali yao.

Alisema maafisa wengi wa polisi wanaathiriwa na tatizo la msongo wa mawazo “kwa sababu wanalipwa mishahara duni.”

“Serikali ya Dkt Ruto itaimarisha mazingira ya utendakazi wa maafisa wetu wa polisi ili kuwapa moyo wa kufanya kazi kwa bidii,” Bw Gachagua akasema.

Mbunge huyo aliapa kwamba kama Naibu Rais, atalinda masilahi ya watu wa Mlima Kenya ndani ya serikali ya Dkt Ruto.

“Nitahakikisha kuwa kuna uwakilishi mzuri wa watu kutoka Mlima Kenya katika serikali ya Kwanza Kwanza. Kwa hivyo, msiwe na wasiwasi,” Bw Gachagua akasema.

Kwa upande mwingine aliwahakikishia walimu kwamba hawatahamishwa kufanya kazi nje ya eneo hilo la Mlima Kenya.

“Walimu wanafaa kufanya kazi katika kaunti walikozaliwa ili waweze kulinda familia zao,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Adai Joho amzuia kuonana na Raila

Wawaniaji Azimio wakimbilia Raila

T L