• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 9:50 AM
BAHARI YA MAPENZI: Ndoa huyumba pale mume na mke wote ni vichwa ngumu

BAHARI YA MAPENZI: Ndoa huyumba pale mume na mke wote ni vichwa ngumu

NA BENSON MATHEKA

NI kawaida ya tofauti kuzuka baina ya wanandoa.

Hii hutokea hata kwa wale ambao wamekuwa kwa ndoa kwa miaka mingi.

Kuna wanaovunja ndoa yao kwa sababu ya kutofautiana na kuna wanaotumia hekima kutatua tofauti hizi na kuzifanya nguzo ya kujenga ndoa yao.

Kinachofanya tofauti kati ya mume na mke kuvunja ndoa ni mmoja – kuwa na msimamo mkali.

Hawa ni watu walio na moyo mgumu wasioweza kunyenyekea, kushukuru kwa mema wanayotendewa na wachumba wao au kuomba msamaha wanapowakosea.

Kuna wasioweza kusamehe waume au wake wao na hii ni sumu kwa ndoa. Wanachosahau ni kwamba hakuna malaika katika dunia hii.

Mtu yeyote anaweza kukosa. Watu kama hao wapo na wanawakosesha raha wachumba wao na hata kusababishia masononeko katika maisha yao ya ndoa.

Mara nyingi wenye tabia hizi huwa wanazidhihirisha baada ya kupata watoto wanaowatumia kama mtego wasitalikiwe.

Kile ambacho watu walio na moyo mgumu hawafahamu ni kwamba, kunyenyekea na kushukuru kunajenga ndoa na tabia yao inaibomoa.

Watu walio na moyo kama chuma wanachoma ndoa zao na hawawezi kuzidumisha. Watu walio na hulka hiyo huwanyima waume na wake wao raha waliyokusudia na kutarajia walipooana.

Kuna wanaume walio na msimamo mkali hivi kwamba hawawezi kupongeza wake wao wakisema kufanya hivyo kutawafanya wawadharau. Huo ni upuzi. Msheheneze mke wako pongezi na shukrani na utanogeza penzi.

Mwanamume asiyepongeza mkewe kwa mapishi bomba hawezi kutarajia mkewe ampongeze kwa kumnunulia zawadi.

Iwapo haupongezi mtu wako usitarajie naye akupongeze. Ni hali ya nipe nikupe. Jifunze kuhongera mume na mkeo hata kama ni haki yake kukufanyia unayochukulia kama kawaida.

Naam, legeza msimamo wako kwa mambo yanayoweza kuzua vurugu na kuwa sumu kwa ndoa. Usiwe pharaoh anayesubiri maafa yatokee ili aweze kulegeza msimamo. Mume, omba mkeo msamaha unapomkosea badala ya kumfokea na kumkumbusha kuwa wewe ni kichwa cha boma. Wanaojua siri hii wamenawiri licha ya changamoto za ndoa zinazoripotiwa kila sehemu ya ulimwengu.

Unaweza kufanya ndoa yako kuwa tofauti kwa kutokuwa na moyo mgumu kwa mambo yanayofanya utofautiane na mume au mkeo.

Hakuna mipaka ya shukrani miongoni mwa wanandoa kwa hivyo mtu hafai kuchoka kumpongeza mume au mkewe na hii haiwezekani kwa walio na misimamo mikali au wanaokumbushana makosa ya awali kila wanapotofautiana.

Mke, mshukuru mumeo kwa kuwa na bidii na kukidhi mahitaji ya familia, mume mshukuru mkeo kwa kutunza watoto na kukuvumilia katika maisha.

Shukuru kwa kumpata mume na mke mwaminifu katika ulimwengu uliojaa uzinifu, mshukuru mume au mkeo kwa kukubali ilhali kuna watu wengi warembo na jamaa ambao angechagua na zaidi ya yote mshukuru mkeo au mumeo kwa kufumbia macho udhaifu na mapungufu yako mengi na kukupenda.

Kuwa na msimamo mkali kunafanya mtu asione chochote cha kumshukuru mume au mke wake. Hauwezi kushikilia msimamo wako hadi kuumiza mume au mkeo na kisha hudai mapenzi kutoka kwake.

  • Tags

You can share this post!

Mjane asimulia jinsi Al-Shabaab walivyofanya maisha yake...

Gachagua: Watu kutoka Nyeri huchangamkia kazi kama fisi kwa...

T L