• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Gavana Nyong’o hatarini kukamatwa kwa kukaidi seneti

Gavana Nyong’o hatarini kukamatwa kwa kukaidi seneti

Na VICTOR RABALLA

GAVANA wa Kisumu Anyang Nyong’o anakabiliwa na tishio la kukamatwa endapo atafeli kufika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Afya kuelezea jinsi serikali yake ilitumia Sh238 milioni ilizopokea kufadhili mipango ya kupambana na janga la Covid-19.

Akitoa onyo hilo, Karani wa Seneti, Jeremiah Nyengenye, alimtaka gavana huyo kufika mbele ya kamati hiyo Ijumaa saa tatu asubuhi kwa njia ya mtandao wa Zoom.

“Zingatia kwamba kamati hiyo inaweza kukutoza faini isiyopungua Sh500,000 au iamuru ukamatwe na polisi ikiwa utafeli kufika mbele yake siku na saa iliyotajwa katika agizo hili,” akasema.

Bw Nyengenye pia alisema kuwa Profesa Nyong’o atakuwa amevunja sehemu 27 (1) ya Sheria kuhusu Mamlaka na Hadhi ya Bunge ya 2017. Kulingana na sheria hiyo, Profesa Nyong’o anaweza kuadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh200,000 au kifungo cha miezi sita gerezani au adhabu zote mbili ikiwa atakaidi amri ya kufika mbele ya kamati inayoongozwa na Seneta wa Trans Nzoia Michael Mbito.

Wanachama wa Kamati hiyo wamemsuta Profesa Nyong’o kwa kupuuza mwaliko wa kumtaka afike mbele yao Jumanne wiki iliyopita kujibu maswali kuhusu matumizi ya fedha hizo za Covid-19, yaliyoibuliwa kwenye ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathugu.

Katika ripoti yake, Bi Gathugu alisema kuwa serikali ya kaunti ya Kisumu haikutumia Sh238 milioni bila kufuata kanuni na taratibu za bajeti.

Mkaguzi huyo pia alisema serikali ya Nyong’o ilichanganya fedha za ruzuku ya majukumu maalum na fedha ambazo ilipokea kutoka kwa wafadhili.

Kati ya pesa hizo (Sh238 milioni), Sh159.8 milioni zilikuwa ruzuku ya miradi maalum zilizotolewa na serikali ya kitaifa, Sh7.7 milioni kutoka kwa shirika la DANIDA, Sh68.4 milioni zilizotengewa malipo ya marupurupu ya wahudumu wa afya, Sh50 milioni kutoka kwa mfuko wa ushuru uliokusanywa na serikali ya Kisumu na Sh1.5 milioni ambazo ni ruzuku kutoka vianzo vingine.

You can share this post!

Wezi wa mifugo sasa wageukia teknolojia kuiba, kuhepa polisi

Corona: Idadi ya waliopokea chanjo duniani yafika bilioni