• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Hatimaye Moi atangaza kuwania urais 2022

Hatimaye Moi atangaza kuwania urais 2022

Na WANDERI KAMAU

SENETA Gideon Moi wa Baringo hatimaye ametangaza rasmi kuwa atawania urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Akihutubu kwenye hafla maalum ya kutoa shukrani katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Ruth Kiptui, Ijumaa, eneo la Baringo Kaskazini, Gideon alisema atafanya kampeni kali kuhakikisha amemrithi Rais Uhuru Kenyatta.

Hii ni mara ya kwanza kwa Gideon kutangaza hadharani kuwa atakuwa kwenye kinyang’anyiro cha urais.

“Nitakuwa debeni. Ninataka kuhakikisha nimemrithi Rais Kenyatta,” akasema Gideon, ambaye pia ndiye kiongozi wa chama cha Kanu.

Gideon alitoa tangazo hilo baada ya kushinikizwa na mbunge William Cheptumo (Baringo Kaskazini) kutoendelea kutapatapa kuhusu jambo hilo na badala yake kutangaza msimamo wake wazi.

Hata hivyo, kulingana na wadadisi wa siasa, tangazo la Gideon linaonekana kuvuruga mikakati ya kisiasa katika muungano wa Okoa Kenya Alliance (OKA), ikizingatiwa kuwa bado haujamtangaza kiongozi atakayewania urais kwa tiketi yake.

Muungano huo unawashirikisha Gideon, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper) na Seneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya).

Wadadisi pia wanasema tangazo hilo linaonekana kusukumwa na hatua ya Rais Kenyatta kuonekana kumpendelea Gideon kuwa mrithi wake, ikilinganishwa na vigogo wengine ambao wametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo.

Kufuatia mwelekeo huo, wadadisi wanatabiri “mwanzo wa kivumbi kikali cha kisiasa” kati yake na Naibu Rais William Ruto kwenye ubabe wa kisiasa katika Bonde la Ufa.

You can share this post!

Kauli za Uhuru zatishia Raila

Ruto hatimaye afafanua mfumo wa ‘Bottom-up’