• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 6:30 PM
IEBC kutathmini tisa wanaotaka kumrithi Joho

IEBC kutathmini tisa wanaotaka kumrithi Joho

VALENTINE OBARA NA KEVIN ODIT

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), imepanga kutathmini stakabadhi za wawaniaji tisa wa ugavana Mombasa kuanzia Jumamosi.

Shughuli hiyo iliyopangiwa kufanyika kwa siku nne, itapelekea wapigakura kujua kuhusu ikiwa wanasiasa wanaowashabikia watakubaliwa kushiriki katika uchaguzi wa kurithi kiti cha Gavana Hassan Joho, ifikapo Agosti 9.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na IEBC, walioorodheshwa kuwa wamevuka awamu ya kwanza kuelekea kwa uchaguzi huo ni Bw Daniel Munga Kitsao ambaye ni mwaniaji huru, aliyekuwa seneta wa Mombasa, Bw Hassan Omar, Naibu Gavana wa Mombasa, Dkt William Kingi (PAA), na aliyekuwa mbunge wa Nyali, Bw Hezron Awiti (VDP).

Wengine ni Bw Anthony Chitavi (UDP), Bw Said Abdalla (Usawa Kwa Wote), Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir (ODM), Bw Shafii Makazi (UPIA), na aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko (Wiper).

Mahakama ilikuwa imetoa agizo la muda kwa IEBC isiidhinishe uwaniaji wa Bw Sonko hadi kesi zinazompinga zikamilike. Kesi hizo zinazohusu uadilifu wake zilikabidhiwa kwa Jaji Mkuu Martha Koome.

Mnamo Jumapili, baadhi ya wawaniaji ubunge waliwasilisha stakabadhi zao kwa afisi za IEBC ili kuidhinishwa.

Wawaniaji huru walikabiliwa na wakati mgumu huku baadhi yao wakilazimika kurudi kujipanga upya baada ya kupata waliwasilisha stakabadhi visivyo.

Katika eneobunge la Jomvu, Bw Kajembe Abdulrahim Ramadhani, alitakiwa kusahihisha orodha ya wapigakura wanaounga mkono azma yake.

Hii ni baada ya maafisa wa IEBC kubainisha kuwa majina aliyowasilisha yalikuwa ya wapigakura ambao ni wanachama wa vyama tofauti.

Ilihitajika mgombea huru aungwe mkono na wapigakura wawili wasio wanachama wa chama chochote cha kisiasa nchini, akafanikiwa kufanya hivyo na kuepuka kufungiwa nje.

Katika eneobunge la Nyali ambalo lilivutia idadi kubwa zaidi ya wawaniaji huru baina ya maeneobunge yote Mombasa, baadhi yao walipatikana hawana vyeti vilivyohitajika.

Walipewa muda kusahihisha kasoro zilizopatikana.

“Wito wangu kwa vijana ni kuwa washiriki shughuli hii ya uchaguzi kwa busara ili wawe miongoni mwa wale watakaochangia kuleta uongozi bora hasa katika eneobunge la Nyali,” akasema Bw Joshua Ndere, mmoja wa wawaniaji huru.

Bw Eric Gitonga, ambaye pia ni mwaniaji huru wa ubunge Nyali, alikiri haitakuwa rahisi kupambana na wawaniaji wanaofadhiliwa na vyama.

Mbunge wa eneo hilo, Bw Mohamed Ali, alitarajiwa kuwasilisha stakabadhi zake baadaye mchana.

Bw Ali alikuwa ameshinda kiti hicho kama mwaniaji huru katika uchaguzi wa 2017 lakini sasa amejiunga na Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Huzuni kijana akifia kilabuni

Uhuru, Raila waomboleza kifo cha mbunge wa Rabai

T L