• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Jamhuri ya mwisho ya Uhuru

Jamhuri ya mwisho ya Uhuru

Na LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta leo anaongoza nchi kwa mara ya mwisho kuadhimisha Sherehe ya Jamhuri kabla ya kung’atuka madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.

Rais Kenyatta ameongoza sherehe zote za Jamhuri kila Desemba 12 tangu 2013. Hata hivyo, Rais huenda akaondoka mamlakani bila kutekeleza nyingi ya ahadi ambazo amekuwa akizitoa katika hotuba zake wakati wa maadhimisho ya sherehe ya Jamhuri.

Disemba 2013, Rais Kenyatta aliongoza taifa kwa mara ya kwanza kuadhimisha sherehe ya Jamhuri miezi minane baada ya kuapishwa kuchukua hatamu za uongozi wa nchi kutoka kwa mtangulizi wake Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

? Ahadi

Katika hotuba yake ya kwanza, Rais alimiminia sifa tele Katiba ya 2010 huku akiitaja kama urithi ambao tunafaa kuulinda. Lakini katika hotuba yake ya Disemba 12, 2020, Rais Kenyatta alitumia muda mwingi kuelezea Wakenya ni kwa nini Katiba ilihitaji kufanyiwa marekebisho kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) ambao baadaye ulitupiliwa mbali na mahakama.

Katika hotuba yake ya kwanza Rais Kenyatta pia alitangaza vita vikali dhidi ya wafisadi huku akionya watumishi wa serikali wanaotumia vibaya mali ya umma. Lakini Januari mwaka huu, Rais Kenyatta alionekana kusalimu amri baada ya kukiri kwamba zaidi ya Sh2 bilioni fedha za umma zinaibiwa kila siku.

Katika hotuba ya Rais Kenyatta ya Disemba 12, 2014, Rais Kenyatta alitumia dakika kadhaa kuelezea manufaa ya mfumo wa ugatuzi nchini. Kiongozi wa nchi aliahidi kwamba serikali ya Jubilee ingeongeza mgao kwa serikali za kaunti kutoka kiwango cha chini kilichowekwa na Katiba cha asilimia 15 ya mapato ya kitaifa hadi asilimia 45.

“Katiba imeweka kiwango cha chini cha mgao wa mapato ya nchi kwa kaunti kuwa asilimia 15. Lakini lengo langu ni kuona huduma zikiboreshwa na maendeleo kuongezeka katika kaunti. Hivyo tutaongeza mgao hadi asilimia 45 ya fedha za bajeti,” akasema Rais Kenyatta.

Lakini ripoti iliyotolewa mwezi uliopita na Tume ya Kugawa Rasilimali za Umma (CRA) inaonyesha kuwa mwaka wa matumizi ya fedha wa 2015/2016 ndio serikali za kaunti zilipewa mgao wa juu zaidi wa asilimia 22.5 ya mapato ya kitaifa.

Serikali ya Jubilee pia imekuwa ikilaumiwa na magavana kwa kuchelewesha fedha hivyo kutatiza huduma katika kaunti.Rais Kenyatta pia aliahidi kuanzishwa kwa mradi wa unyunyiziaji maji wa ekari 1,000,000 katika eneo la Galana-Kulalu kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.

Kufikia sasa ni ekari chini ya 10,000 zilizo na kilimo cha unyunyiziaji maji katika eneo la Galana Kulalu na Wakenya hawajaanza kuvuna matunda yake. Rais tayari ametangaza baa la njaa kuwa janga la kitaifa na takribani Wakenya 2.3 kutoka Kaunti 23 wanahitaji chakula kwa dharura.

Katika hotuba ya Disemba 12, 2017, Rais Kenyatta aliahidi kuwa kufikia mwishoni mwa utawala wake mwaka ujao, zaidi ya familia 500,000 zitakuwa zimekabidhiwa nyumba bora kwa bei nafuu. Ahadi sawa pia ilitolewa katika hotuba ya sherehe za Jamhuri ya 2019 ambapo alisema kuwa nyumba hizo zimeanza kujengwa katika kaunti mbalimbali nchini.

Kulingana na waziri wa Uchukuzi na Makazi James Macharia, serikali imefanikiwa kujenga nyumba nafuu 186,000 ndani ya miaka minane iliyopita. Hiyo inamaanisha kwamba Rais Kenya huenda akaondoka mamlakani bila kukamilisha nyumba 314,000 zilizosalia.

Siku ya Madaraka huadhimishwa kukumbuka siku ambayo Kenya ilipata uhuru wa ndani mnamo Juni 1, 1963. Rais Kenyatta atang’atuka mamlakani bila kufikisha SGR mpakani Malaba kama alivyokuwa ameahidi.? Rais Kenyatta pia ataachia Wakenya mzigo wa madeni na gharama juu ya maisha.

You can share this post!

Ruto ni maarufu kuliko raila eneo la Mlimani’

Khalwale mfia Ruto anayeamini ataingiza Mudavadi katika...

T L