• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 5:46 PM
Jinsi Wajackoyah alivyojimaliza kisiasa ghafla

Jinsi Wajackoyah alivyojimaliza kisiasa ghafla

NA WANDERI KAMAU

HATUA ya mwaniaji urais kwa chama cha Roots Party, Prof George Wajackoyah kutangaza kuwa anamuunga mkono mwaniaji urais wa muungano wa Azimio-One Kenya, Bw Raila Odinga, imevunja wimbi jipya la kipekee la kisiasa lililokuwa limevuma kote kote.

Msimamo huo mpya wa Prof Wajackoyah, ulithibitishwa Jumatano na mgombea-mwenza wake, Bi Justina Wamae, aliyekubali madai yaliyoibuka kwamba mwaniaji huyo wa urais amekuwa akimuunga mkono Bw Odinga.

“Ni kweli kuwa mkubwa wangu (Prof Wajackoyah) anaunga mkono Azimio. Hata hivyo, hatujajadiliana hilo kama chama. Hatujakubaliana na pia sijaulizwa kuhusu msimamo wangu. Ikiwa hali itatulazimu kufuata mkondo huo, mimi nitaunga mkono mrengo pinzani (Kenya Kwanza). Licha ya hayo, bado hatujajadiliana rasmi kama chama,” akasema Bi Wamae.

Tuhuma za Prof Wajackoyah kumuunga Bw Odinga zilianza kujitokeza mwishoni mwa mwezi Juni, aliposema kuwa hana tatizo lolote kushirikiana kisiasa na Bw Odinga.

Alitoa kauli hiyo alipofanya mikutano kadhaa ya kampeni jijini Kisumu.

“Agwambo (Raila) amenituma. Ameniambia kuhusu mahali ninapofaa na nisipofaa kwenda. Ameniruhusu kumfanyia kampeni hadi tupate ushindi. Ikiwa hutanipigia kura, basi heri umpigie kura. Ushindi wa mmoja wetu utakuwa ushindi wetu sote,” akasema msomi huyo kwa lugha ya Dholuo.

Kwa mara kadhaa, imemlazimu Prof Wajackoyah kukanusha madai ya kuwa “mradi wa kisiasa” wa serikali na Bw Odinga.

Madai hayo yalitolewa na Naibu Rais William Ruto na washirika wake, waliodai kuwa Prof Wajackoyah anafadhiliwa kisiri na serikali ili kugawanya kura na kuvuruga ufuasi wake.

Hapo jana Alhamisi, wadadisi wa siasa walisema kuwa msomi huyo atakuwa amewasaliti maelfu ya wafuasi wake, waliomwona kuwa “dalili ya mapambazuko mapya ya kisiasa nchini”.

Baadhi ya makundi ya watu waliojitokeza kumuunga mkono ni watu wanaofuata taratibu na imani za jamii ya Kirasta, wengi wakimtaja mwaniaji huyo kama “mkombozi wao.”

“Hatimaye tumepata mtu atayakekuwa sauti yetu,” akasema Bw Paul Musyoki, mfuasi wa itikadi za Kirasta.

Mbali na watu hao, alizua msisimko wa aina yake miongoni mwa Wakenya, kufuatia baadhi ya ajenda na mapendekezo yaliyokuwa kwenye manifesto yake.

Baadhi ya ahadi alizotoa ni kuhalalisha ukuzaji, matumizi na uuzaji wa bangi kama njia ya “kuiwezesha Kenya kupata fedha za kulipia deni lake la kitaifa”.

Ijapokuwa wadadisi wanasema ingeuwa vigumu kwake kutekeleza baadhi ya ahadi alizotoa, amepoteza nafasi nzuri ya kuweka kwenye mizani ushawishi wake wa kisiasa.

“Mwelekeo huo mpya ni pigo kubwa kwa wafuasi wa Profesa Wajackoyah, hasa walioeleza kuchoshwa na viogogozi kama Raila na Ruto, ambao wamekuwa kwenye ulingo wa siasa kwa muda mrefu,” asema Bw Dismus Mokua, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamke alilia korti imsaidie kupata Sh29m kutoka kwa sacco

Chebukati awasihi Wakenya kuombea maafisa wa IEBC

T L