• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 8:50 AM
Jubilee: Kanini nje, Kioni ndani tena

Jubilee: Kanini nje, Kioni ndani tena

NA RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu iliurejeshea mrengo wa mbunge wa zamani wa Ndaragwa Jeremiah Kioni uongozi wa chama cha Jubilee, siku tatu baada ya jopo la kuamua mizozo ya vyama vya kisiasa kuutambua mrengo wa mbunge maalum Sabina Chege.

Akisitisha hatua ya Bi Chege na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Kanini Kega kutwaa uaongozi wa Jubilee, Jaji Asenath Ongeri alisema Bw Kioni na wenzake waendelee kukiongoza chama cha Jubilee hadi rufaa iliyowasilishwa isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Ongeri alisema Bw Kioni aendelee kuhudumu kulingana na Gazeti rasmi la Serikali la Machi 22, 2023.

Pia jaji huyo alisitisha kutekelezwa maelekezo yaliyoko kwenye Gazeti rasmi la Serikali la Julai 12, 2023 lililowatambua Kega na Chege kuwa viongozi wa Jubilee.

Sasa Jaji huyo amerejesha uongozi wa Jubilee kwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na Bw Kioni kama Katibu wake Mkuu.

Jaji Ongeri aliratibisha rufaa hiyo ya kutatua mzozo wa chama cha Jubilee isikilizwe Julai 26, 2023.

Katika rufaa hiyo Mabw Kioni, naibu wa mwenyekiti wa Jubilee David Murathe na Kagwe Gichohi waliomba Jaji Ongeri asitishe uamuzi wa Julai 10 uliowapokonya chama hicho na kuratibisha kutimuliwa kwao chamani.

Wakili Jackson Awele alisema wanachama watatu wa jopo la kuamua mizozo ya kisiasa (PPDT) walikubaliana na Bw Kioni kwamba hawakupewa fursa ya kujitetea na kamati ya nidhamu ya chama cha Jubilee iliyoendeleza ‘ukatili’ huo katika mkahawa mmoja mjini Naivasha.

Wanachama wanne wa jopo hilo la watu saba walitofautiana na mrengo wa Bw Kioni na kuupokonya uongozi wa chama cha Jubilee.

Kufuatia uamuzi huo wa PPDT, msajili wa vyama katika afisi ya mwanasheria mkuu Anne Nderitu alichapisha katika Gazeti la Serikali toleo la Julai 12, 2023 mabadiliko ya uongozi katika Jubilee kwa kutambua mrengo wa Kanini Kega.

  • Tags

You can share this post!

Lenolkulal yuko na kesi ya kujibu katika ufisadi wa Sh84.6...

Zetech Sparks yalenga kusuka kikosi ipate kani kali za...

T L