• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 6:55 AM
Jumwa ajipiga kifua baada ya ‘Reggae’ kuzimwa

Jumwa ajipiga kifua baada ya ‘Reggae’ kuzimwa

Na WAANDISHI WETU

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, ameungana na wabunge wenzake wa Pwani waliopinga hadi mwisho refarenda kusherehekea kuharamishwa kwa Mswada wa Kurekebisha Katiba (BBI).

Bi Jumwa ni miongoni mwa wabunge wachache wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto ambao walipiga kura ya ‘la’ wakati mswada huo wa Mpango wa Maridhiano ulipofikishwa bungeni wiki mbili zilizopita.

Pamoja na mwenzake wa Nyali, Bw Mohammed Ali, na Mwakilishi Mwanamke wa Kaunti ya Tana River, Bi Rehema Hassan, wanaamini uamuzi wa mahakama umewaondolea lawama.

Bi Jumwa aliwakejeli viongozi wa Kaunti ya Kilifi ambao ni mawakili kwa kuunga mkono BBI. Alikuwa akiwarejelea Gavana Amason Kingi, Senata Stewart Madzayo, Mbunge wa Rabai William Kamoti na spika wa bunge la Kilifi, Bw Jimmy Kahindi.

“Wametushangaza kwa sababu raia wa kawaida kama Aisha Jumwa ambaye hana ufahamu wowote wa sheria aliona BBI ina kasoro,” akasema.

Akizungumza eneo la Rabai wikendi, Bi Jumwa aliwasuta wenzake wa Tangatanga waliopigia mswada huo kura ya ‘ndiyo’ bungeni akisema kuwa lazima wawe na msimamo.

Kwa upande wake, Bw Mohammed alirejelea hotuba yake ya awali ambapo alikuwa amesomea waumini Biblia, kitabu cha Isaya 10:1-4, inayoonya kuhusu hasira kali ya Mungu dhidi ya viongozi wanaopitisha sheria za kudhulumu wanyonge.

“Niliwaonya hawakusikia. Mungu ni mkuu, hutoa haki kwa wanyonge. Mungu abariki wahudumu wote wa mahakama. BBI haina nguvu mbele ya haki,” akasema Bw Mohammed, kupitia mtandao wa Twitter.

Hata hivyo, Gavana wa Tana River, Bw Dhadho Godhana alisema wapinzani wa BBI hawatasherehekea kwa muda mrefu kwa vile ana hakika kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu ulikuwa na makossa.

Bi Rehema Hassan alisema wanafahamu fika uwezekano kuwa serikali huenda ikatumia kila njia hadi katiba irekebishwe, lakini uamuzi wa mahakama ni wa kihistoria unaostahili sifa.

Mbunge Mwakilishi wa Kaunti ya Kwale, Bi Zuleikha Hassan alikosoa uamuzi wa mahakama akasema ni pigo kwa mafanikio yaliyotarajiwa kaunti hiyo.

Kulingana naye, changamoto kama vile ukabila na ukosefu wa haki katika ugavi wa rasilimali zitaendelea ikiwa katiba haitarekebishwa ilivyopangwa.

  • Tags

You can share this post!

Serikali kuwasilisha rufaa kortini leo

Wetang’ula awatetea majaji 5 kuhusu BBI