• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Kalonzo aonekena kujaa masumbuko

Kalonzo aonekena kujaa masumbuko

NA BENSON MATHEKA

VIGOGO wa siasa wanapoendelea kujipanga kwa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka bado anatapatapa gizani, hali ambayo imewaacha wafuasi wake wamechanganyikiwa.

Baada ya mwaniaji urais wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga kukataa kumteua naibu wake mnamo Jumatatu, Bw Musyoka alisema amejiondoa katika muungano huo na atawania urais kivyake kwa chama cha Wiper.

Kabla ya kuingia Azimio, Bw Musyoka alikuwa akisisitiza Bw Odinga alifaa kumuunga mkono yeye, na hata akasema atakuwa ‘mtu mjinga zaidi duniani’ kumuunga mkono Bw Odinga kuwania urais.

Hata hivyo alivunja msimamo huo alipojiunga na Azimio na kutangaza kumuunga mkono Bw Odinga kuwania urais kwa kile alisema ni hakikisho la Rais Uhuru Kenyatta kuwa angelinda maslahi yake.

Akiwa Azimio alisisitiza ndiye chaguo faafu la mwaniaji mwenza na hangekubali cheo kingine.

Ndiposa mnamo Jumatatu alitangaza atawania urais baada ya Bw Odinga kukataa kumteua mwenza wake.

Bw Musyoka alipokuwa akitangaza kujiondoa Azimio na kuwa atawania urais kwa tiketi ya Wiper alisema atachukua muda wa wiki moja kutafakari, ishara kuwa hajafikia uamuzi wa mwisho, na bado anaweza kurudi Azimio wakati wowote.

Alipokuwa akimtangaza Bi Martha Karua kuwa mwenza wake, Bw Odinga alisema Bw Musyoka ametengewa wadhifa wa Mkuu wa Mawaziri katika serikali ya Azimio iwapo watashinda uchaguzi wa Agosti 9.

Seneta wa Makueni, Mutula Kilonzo Junior anasema Bw Musyoka alipuuza ahadi hiyo kwa vile utimizaji wake utakuwa kwa hiari ya Bw Odinga: “Walimtengea wadhifa wa Mkuu wa Mawaziri lakini ni wadhifa usio katika Katiba na pia hauko katika mkataba wa Azimio. Ni wadhifa hewa tu.”

Wachanganuzi wa siasa wanasema tangazo la Bw Musyoka kuwa atawania urais ni vitisho ili aweze kushinikiza ahadi hiyo ijumuishwe kwenye mkataba wa Azimio kama hakikisho kuwa hatapigwa chenga na Bw Odinga akiwa rais, kama ambavyo amekuwa akidai kufanyiwa mbeleni.

MKATABA

Duru zinaeleza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kinara huyo wa Wiper kuondoa vitisho vyake vya kuwania urais na kumuunga mkono Bw Odinga iwapo ahadi yake ya kupewa wadhifa wa Mkuu wa Mawaziri itawekwa kwenye mkataba wa Azimio.

Wadadisi wanasema japo Bw Musyoka anadai atagombea urais, azma yake ni hewa tu kutokana na sababu za kisheria kuhusu miungano ya kisiasa.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Anne Nderitu anasema Bw Musyoka hawezi kujiondoa katika Azimio la Umoja One Kenya kabla ya kukamilisha mfumo wa kutatua mizozo ndani ya muungano huo: “Kutia sahihi mkataba wa muungano kunamaanisha wahusika walisoma mkataba na kuuelewa kabla ya kuukubali, na hivyo ni juu ya muungano husika kutatua malalamishi ya wanachama.”

Kulingana na mkataba wa Azimio la Umoja One Kenya, vyama tanzu haviwezi kujiondoa miezi sita kabla ya uchaguzi na miezi sita baada ya uchaguzi, hali ambayo inamfunga Bw Musyoka minyororo ndani ya Azimio.

“Kalonzo anasumbuka tu bure kwa kuwa amewekwa pingu katika Azimio,” asema Wakili Steve Ogolla.

“Kwa kutisha kuwania urais, Kalonzo anafanya hesabu za kuwanyima wagombeaji wakuu kura za Ukambani ili kuwe na awamu ya pili ya kura ambapo atakuwa na uamuzi wa mshindi. Lakini anaweza kujipata kwenye baridi kwa kuwa mshindi anaweza kupatikana katika duru ya kwanza. Kwa sasa hawezi hata kujiunga na Kenya Kwanza kwa kuwa nyumba ya Ruto tayari imejaa. Yumo katika hali tata,” asema Bw Karanja.

Wakosoaji wa Bw Musyoka wanawalaumu maseneta Mutula na Enock Wambua wa Kitui pamoja na wakili Dan Maanzo wakidai ndio wanamshinikiza kufanya baadhi ya maamuzi ya kukanganya kwa ajili ya maslahi yao ya kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

Roho mkononi wanatenisi ya mezani wakingoja usaidizi...

VALENTINE OBARA: Juhudi za kuzima uhalifu zisiwe...

T L