• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Kalonzo pabaya Ruto akiweka mikakati kupenya ngome yake

Kalonzo pabaya Ruto akiweka mikakati kupenya ngome yake

NA ONYANGO K’ONYANGO

INGAWA anachukuliwa kuwa tishio la kisiasa kwa Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027, kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka huenda akakabiliwa na hali ngumu katika ngome yake ya Ukambani.

Tofauti na ilivyokuwa katika muhula wa pili wa chama cha Jubilee eneo hilo lilipokuwa na waziri mmoja Dkt Monica Juma ambaye amezaliwa Kitui na kuolewa Murang’a, Rais Ruto amezawidi eneo hilo nafasi tatu za mawaziri ambao ni Dkt Alfred Mutua wa Mashauri ya Kigeni, Peninah Malonza wa Utalii huku akimhifadhi Dkt Juma kama mshauri wake wa masuala ya Usalama, wadhifa sawa na uwaziri.

Wakati huo huo, eneo hilo lina makatibu watatu wa wizara ambao ni Teresia Mbaika Malokwe (Masuala ya Baraza la Mawaziri), Veronica Mueni Nduva (Jinsia) na Jonathan Mueke (Michezo na Sanaa), kitu ambacho wachambuzi wanasema ni njama ya kiongozi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kurai Ukambani kumuunga mkono.

Katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, kwa usaidizi wa waziri Mutua na mwenyekiti wa UDA Johnson Muthama, Rais Ruto alipata kura 250,070 kutoka kaunti tatu za Ukambani ambazo ni Machakos, Kitui na Makueni ikiwa ni asilimia 24.1 ya kura zote zilizopigwa ikilinganishwa na kura 192,646 ambazo Jubilee ilipata Ukambani katika uchaguzi mkuu wa 2017 ikiwa ni asilimia 16.6.

Baada ya ushindi wa Dkt Ruto, baadhi ya viongozi kutoka eneo hilo wamehamia muungano wa Kenya Kwanza nyuma ya Bw Muthama ambaye amekuwa akiandaa mikutano kila wikendi inayochukuliwa ya kupanga siasa.

Viongozi kama aliyekuwa Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana, aliyekuwa seneta wa Kitui David Musila, wamejiunga na Bw Muthama kuhimiza eneo hilo kuunga utawala wa Rais Ruto.

Jana Jumanne, Bw Muthama alikiri kwamba mikutano hiyo inalenga kuhakikisha chama hicho kimekuwa maarufu katika eneo hilo ambalo kwa miaka mingi limekuwa ni ngome ya Wiper na kuongeza kuwa teuzi zilizofanywa na Rais hazifai kuchukuliwa kama njama ya kuzima umaarufu wa kisiasa wa Bw Musyoka.

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Dalili za ukosaji wa kafeni kwa mraibu

Talaka ya Jubilee na ODM sasa yaiva

T L