• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 5:59 PM
Karua aahidi kuyeyusha umaarufu wa Naibu Rais

Karua aahidi kuyeyusha umaarufu wa Naibu Rais

MWANGI MUIRURI na LEONARD ONYANGO

MGOMBEA mwenza wa urais kwa tikiti ya Azimio, Bi Martha Karua ameapa kumaliza umaarufu wa Naibu wa Rais William Ruto katika eneo la Mlima Kenya ndani ya siku 57 zilizosalia kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Bi Karua alifichua Jumamosi kuwa, muungano wa Azimio la Umoja One Kenya unaandaa kampeni kali ambayo aliifananisha na kimbunga kitachosambaratisha umaarufu wa Naibu wa Rais katika eneo la Mlima Kenya.

Tafiti za kura ya maoni zinaonyesha kuwa, ushawishi wa Dkt Ruto uko juu katika eneo la Mlima Kenya ikilinganishwa na mpinzani wake mkuu Raila Odinga anayewania urais kupitia muungano mkuu wa Azimio.

Ripoti ya utafiti wa Shirika la Infotrak iliyotolewa Jumatano, ilionyesha kuwa, Dkt Ruto atapata asilimia 52 ya kura za Mlima Kenya iwapo uchaguzi utaandaliwa sasa.

Utafiti huo wa Infotrak pia unaonyesha kuwa, Bw Odinga anaungwa mkono na asilimia 27 ya wakazi wa Mlima Kenya.

Tafiti ambazo zimekuwa zikifanywa na kampuni mbalimbali zinaonyesha kuwa, umaarufu wa Bw Odinga umekuwa ukiongezeka kwa kasi katika eneo la Mlima Kenya tangu kumteua Bi Karua kuwa mwaniaji mwenza wake siku 27 zilizopita.

Kufikia mwishoni mwa mwaka 2021, umaarufu wa Dkt Ruto katika eneo la Mlima Kenya ulikuwa zaidi ya asilimia 80.

Tangu kuteuliwa kuwa mwaniaji wa Bw Odinga, Bi Karua amekuwa akizunguka katika eneo la Mlima Kenya kuvumisha muungano wa Azimio.

Mnamo Jumamosi, Bi Karua alizuru Kaunti za Murang’a na Nyeri ambapo alipigia debe muungano wa Azimio.

“Bado hamjashuhudia kampeni zetu katika eneo la Mlima Kenya kufikia sasa, kimbunga cha kisiasa kinakuja. Tutatoa kijasho wale wapinzani wetu na wataisha Mlimani,” Bi Karua akasema.

Akiwarai wakazi kumuunga mkono Raila Odinga, Bi Karua aliwataka wakazi wa Mlima Kenya kupiga kura kwa kuzingatia sera badala ya chuki.

“Mnamo 2013, Rais Uhuru Kenyatta aliahidi kuongoza kwa miaka 10 kisha apitishe naibu wake Dkt Ruto. Lakini ahadi hiyo isiwe msingi wa kupigia kura viongozi waasi. Binadamu anaweza kutoa ahadi lakini wakati mwingine inakuwa vigumu kuitekeleza,” akasema Bi Karua alipokuwa akihutubia wagombea wa vyama vilivyo ndani ya muungano wa Azimio katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu (TTC), Murang’a.

Alisema muungano wa Azimio utawatuma maajenti wake kuendesha kampeni ya nyumba hadi nyumba katika eneo lote la Mlima Kenya “ili kuhakikisha Bw Odinga anapata ushindi mkubwa.”

“Vikosi hivyo vya kampeni pia vitahakikisha kuwa wagombeaji viti mbalimbali kwa tiketi za vyama vya kisiasa wanashinda katika uchaguzi wa Agosti 9,” Bi Karua akaeleza.

Bi Karua leo Jumapili atakuwa katika Kaunti ya Uasin Gishu ambapo ni nyumbani kwa Naibu wa Rais Ruto, na ataongoza mkutano wa kisiasa katika uwanja wa Huruma.

Kulingana na mkurugenzi wa kampeni katika Jubilee, Kanini Kega, Rais Uhuru Kenyatta atakuwa anafanya ziara za mara kwa mara katika eneo la Mlima Kenya kuzindua miradi ya maendeleo katika juhudi za kuvumisha Azimio.

Kumekuwepo mjadala mkali ikiwa Rais Kenyatta anafaa kumpigia debe Bw Odinga katika eneo la Mlima Kenya au la.

Wanaopinga wanasema kuwa hatua hiyo huenda ikasababisha Bw Odinga kupoteza kutokana na imani kwamba, umaarufu wa Rais Kenyatta katika eneo la Mlima Kenya umedorora.

Rais Kenyatta amekuwa akimsaidia Bw Odinga chini kwa chini kwa kushawishi wanasiasa kujiunga na Azimio.

Mnamo Jumamosi, Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui alifichua kuwa wanasiasa kutoka eneo la Mlima Kenya wanatarajiwa kugura Kenya Kwanza na kujiunga na Azimio kabla ya Agosti 9.

  • Tags

You can share this post!

Jepchirchir ajikwaa wakati wa mbio za New York Mini 10K

Mwigizaji ashtakiwa kwa kushindwa kulipa bili ya Sh152,550

T L