• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Karua aonya kuhusu njama ya kuahirisha kura

Karua aonya kuhusu njama ya kuahirisha kura

Na MARY WANGARI

KIONGOZI wa Narc Kenya, Bi Martha Karua amepuuzilia mbali uwezekano wa kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2022 kutokana na janga la Covid-19.

Alisisitiza kwamba Katiba hairuhusu serikali inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, kuongeza muda wa utawala wake.“Hairuhusiwi kikatiba. Serikali haiwezi kutumia janga kuendeleza utawala wake. Ni sawa na kuongeza muda wa mateso kwa Wakenya na kutumia fedha za umma kujitajirisha.”

“Tunahimiza raia waamke na kukomesha hila hiyo. Serikali hii ni sharti ifahamu kwamba Wakenya hawatavumilia usaliti mkuu ambao ni mapinduzi ya kikatiba. Kinachoendelea ni mapinduzi ya katiba na ni sharti tuyakomeshe,” alisema.

Alitaja serikali kama chanzo kikuu cha matatizo yanayowakumba Wakenya wakati huu wa mabadiliko ya hali ya anga na janga la Covid-19.

Kulingana naye, serikali inayotarajiwa kusuluhishia wananchi matatizo yao, sasa imegeuka kiini cha matatizo hayo wakati huu wa virusi vya corona na msimu wa mvua.

Aliwashutumu wahusika wakuu katika Kamati ya Kitaifa kuhusu Usalama na Kamati ya Kudhibiti Covid-19 kwa kuwaadhibu wakazi katika kaunti tano zilizofungwa, wanaohangaika kufika nyumbani jioni kufuatia kafyu ya mapema.

“Acheni kuwapiga vita Wakenya. Mikakati ya kurahisisha usafiri ibuniwe kwa kuzingatia changamoto za usafiri wa umma na ujenzi wa barabara unaoendelea jijini,” alisema.

Wakili huyo vilevile aliikosoa Wizara ya Usalama wa Ndani inayoongozwa na Dkt Fred Matiang’i kufuatia kisa cha hivi majuzi, ambapo wakazi kutoka kaunti hizo tano zilizofungwa walilazimika kukaa barabarani kwa saa kadhaa kwa kukiuka kafyu ya mapema.

Alisema kuwa maafisa wa polisi hawana mamlaka kisheria kuwaadhibu wanaokiuka saa za kafyu akisema ni mahakama tu inayoweza kutoa adhabu.

“Ingekuwa mimi ningesaidia watu kufika nyumbani hasa waliochelewa kwa dakika chache. Ningeelekeza maafisa wangu kuhakikisha hakuna msongamano wa magari kuanzia kituoni hadi barabarani.

“Kwa wanaoonekana kana kwamba walichelewa kimaksudi, ningewapa tiketi za kujiwasilisha kortini siku inayofuatia.Huwezi ukaweka watu barabarani hadi usiku. Hujaruhusiwa kisheria kutoa adhabu, ni korti tu inayoweza kuadhibu. Polisi ni sharti waache kutumia vibaya mamlaka yao ya kukamata watu na kugeuka wanaoshutumu, kutoa hukumu na kuadhibu watu,” alisema.

Bi Karua pia alitofautiana na hatua ya kuwafurusha wakazi katika ardhi za umma bila kuwapa notisi wala makao mbadala.Alifafanua kuwa, mbali na virusi hatari vya corona, wahasiriwa wanakabiliwa na tishio la kupata nimonia katika msimu huu wa mvua ya masika pamoja na matatizo mengine ya kiafya kutokana na msongo wa mawazo.

“Serikali inapaswa kuwapa notisi na kuwasaidia wahasiriwa kuhamia makazi mbadala. Hawawezi tu kutoweka. Serikali ilikuwepo watu hao walipokuwa wakijenga makao yao na haikuwakataza wakati huo. Serikali ina wajibu, ikiwa kweli ardhi hiyo ni ya umma inayohitajika sasa kuendelezwa,” akasema.

You can share this post!

Matumaini kaunti ikisaka soko la maembe ng’ambo

Mvutano kati ya Ottichillo na naibu wake wachacha