• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Kauli za Ndii zaashiria kuna nyufa katika Ikulu ya Rais?

Kauli za Ndii zaashiria kuna nyufa katika Ikulu ya Rais?

NA WANDERI KAMAU

MASWALI yameibuka kuhusu ikiwa mwenyekiti wa Baraza la Washauri wa Rais kuhusu Uchumi (CEA), Dkt Dadid Ndii, hatimaye amemgeuka Rais William Ruto na serikali anayoongoza ya Kenya Kwanza.

Hili linatokana na kauli tata ambazo msomi huyo amekuwa akitoa katika siku za hivi karibuni, wengi wakisema kuwa huenda ametofautiana na utawala wa Rais Ruto.

Mnamo Jumanne, Septemba 26, 2023, Dkt Ndii alionekana kumponda Rais Ruto kutokana na ziara nyingi ambazo amekuwa akifanya ng’ambo, akisema Rais anafanya hivyo huku “Kenya ikiendelea kuwaka moto”.

Ijapokuwa hakumtaja Rais Ruto moja kwa moja kwenye ujumbe wake uliojaa kejeli, kauli yake ilionekana kumlenga Rais.

“Unarejea kutoka kuipigia (nchi) debe kimataifa na kupata tumerejea kwenye maandamano na kuwalisha nyati. Bure kabisa!” akasema Dkt Ndii kwenye ujumbe huo alioweka kwenye mtandao wa X.

Kando na ujumbe huo, msomi huyo alizua hisia wiki mbili zilizopita, aliposema kwamba huwa hawaamini wanasiasa.

“Huwa siwaamini wanasiasa, na huwa siiamini serikali. Ikiwa unafanya moja kati ya hayo mawili, wewe ni mjinga.”

Kwenye ujumbe mwingine, mshauri huyo alisisitiza kuwa Kenya iko karibu kufilisika kutokana na deni kubwa la kimataifa linaloiandama.

“Ni kinaya raia kutarajia mabadiliko bila ugumu kwa watu watu walioiingiza Kenya katika madeni kwa muda wa miaka 10. Eti kwa sababu kulikuwa na mchezo uitwao uchaguzi? Tunajielewa kweli.? Niliwaambia miaka miwili iliyopita kwamba Kenya imefilisika. Hakuna kilichobadilika,” akasema Dkt Ndii.

Akaongeza: “Nimeambiwa ninafaa kuwaomba raia msamaha. Sikubaliani na hilo. Jukumu langu katika jamii hii ni kuieleza ukweli kama ulivyo.”

Wadadisi wanasema kauli za msomi huyo zinaonyesha mivutano ya kichinichini iliyo katika serikali ya Kenya Kwanza.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamke amenivutia na ni mrembo mno, nahisi hawezi...

Brian Chira aweka kiburi kando, aomba msamaha kwa...

T L