• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
Kega akemea Msajili kuhusu waasi JP

Kega akemea Msajili kuhusu waasi JP

Na KENYA NEWS AGENCY

MBUNGE wa Kieni Kanini Kega, amemtaka Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu aamrishe viongozi waasi wa Jubilee wasake uongozi upya baada ya kujihusisha na chama kipya cha UDA.

Bw Kega alisema kuwa sheria inaharamisha kiongozi kuvumisha ajenda ya chama kingine ilhali bado hajajiuzulu kutoka kwa chama kilichomdhamini kupata wadhifa anaoushikilia kwa sasa.

Mbunge huyo wa Jubilee ambaye ni mshirika mkubwa wa Rais Uhuru Kenyatta, alitishia kuwasalisha hoja bungeni kutathmini utendakazi wa afisi ya msajili wa vyama vya kisiasa iwapo itaendelea kukimya kuhusu suala hilo.

“Tutajadili utendakazi wenu bungeni kwa sababu yaonekana mnafumbia macho sheria,” akasema Bw Kega aliyekuwa akizungumza katika eneobunge lake wikendi.

“Sheria inasema wazi kuwa iwapo unaendeleza ajenda ya chama kingine badala ya kile ambacho kilikudhamini ili ushikilie cheo chako, basi inafasiriwa kuwa umekihama chama chako,” akaongeza.

Alisisitiza kuwa anatarajia afisi ya msajili wa vyama iwaandikie wabunge waasi wa Jubilee barua za kutotambua vyeti vya ushindi walivyopokezwa baada ya kura ya 2017.

Aidha mbunge huyo anayehudumu kipindi chake cha pili alimkashifu Naibu Rais Dkt William Ruto kwa kulipaka tope jina la Rais Uhuru Kenyatta eneo la Mlima Kenya kuelekea uchaguzi wa 2022.

“Hatutaendelea kumvumilia kwa sababu tunajua Rais ameanzisha miradi mingi ya maendeleo kwa watu wetu na kutenga rasilimali tele kwa wananchi wote kote nchini,” akasema Bw Kega.

Aidha aliwataka viongozi hao waasi ndani ya Jubilee wajiuzulu nyadhifa zao kisha watafute kuchaguliwa upya kwenye nyadhifa wanazoshikilia iwapo wanaamini wao ni maarufu miongoni mwa raia.

Pia alisifu rekodi ya maendeleo ya Rais, akisema ujenzi wa miundombinu unaendelea maeneo mbalimbali nchini, hasa baada ya kuingia kwenye uhusiano wa karibu na kinara wa ODM Raila Odinga kupitia ‘handisheki’ Machi 2018.

Kwa mujibu wa Bw Kega, wabunge wandani wa Rais na wale wanaomuunga Bw Odinga wanatarajiwa watakutana wiki hii ili kujibu madai yaliyotolewa na wabunge waasi kuwa serikali imezembea katika utendakazi wake.

Wakati wa mkutano huo, itabainika kuwa wana idadi halisi ya wabunge wa kuendeleza ajenda ya serikali bungeni na pia watatangaza mikakati yao ya 2022.

You can share this post!

Covid: Wadau wa utalii walalama kubaguliwa

Kanisa linaloruhusu ndoa za watoto lamulikwa na UN