• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Juhudi zilivyofanywa kupata wa kumkabili Nyong’o Agosti

Juhudi zilivyofanywa kupata wa kumkabili Nyong’o Agosti

NA VICTOR RABALLA

JUHUDI zilizotumika kumteua aliyekuwa Naibu Waziri wa Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Bw Ken Obura, kuwa mgombea mkuu wa ugavana katika Kaunti ya Kisumu, hatimaye zimefichuka.

Bw Obura anaungwa mkono na wawaniaji watatu kumkabili Gavana Anyang’ Nyong’o kwenye uchaguzi wa Agosti.

Wawaniaji hao walikubaliana kutowania nafasi hiyo na badala yake kumuunga mkono Bw Obura.

Watatu hao ni aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo, Jack Ranguma, Seneta Fred Outa na aliyekuwa Spika wa Kaunti hiyo, Bw Onyango Oloo.

Duru zilisema mazungumzo hayo yaliendeshwa na wadau mbalimbali ili kuwaleta pamoja viongozi hao.

Ripoti zilieleza kuwa wakati mazungumzo hayo yalipoanza, wanne hao hawakuwa wanaelewana hata kidogo.

“Tulianza katika mazingira magumu sana. Hakuna aliyetaka kuacha kuwania ili kubuni muungano wa pamoja. Ilichukua juhudi nyingi kuwarai kumuunga mkono Bw Obura,” duru zilifichua.

Mikutano kadhaa iliandaliwa katika sehemu tofauti kama Nairobi na Kisumu, kabla ya kikao cha mwisho kufanyika katika Kaunti ya Vihiga, ambapo uamuzi huo ulifikiwa.

Kabla ya viongozi hao kukubaliana kumuunga mkono Bw Obura, kulikuwa na hali ya kutoaminiana baina yao.

Kando na viongozi hao wanne, watu wengine wanaodaiwa kuendesha mazungumzo hayo ni Naibu Waziri katika Wizara ya Ulinzi Peter Odoyo, aliyekuwa Mkuu wa Wafanyakazi katika kaunti hiyo Patrick Ouya, aliyekuwa mbunge wa Kisumu Mashariki Gor Sungu, aliyekuwa Waziri wa Elimu katika kaunti hiyo, Dkt John Ogone na wakili Ken Amondi.

Baadaye, waliagizwa kuwaleta wawakilishi mbalimbali, wakiwemo vijana, wazee na viongozi wa kidini ili kufanikisha makubaliano hayo.

Baadhi ya wanachama hata hivyo walianza kumtuhumu Bw Ouya kama msiri wa Prof Nyong’o kutokana na ukaribu waliokuwa nao hapo awali.

Kwenye mkutano huo wa mwisho uliofanyika wiki mbili zilizopita, wanne hao walikubaliana kwa pamoja kumuunga mkono Bw Obura.

“Kwa mshangao wa kila mmoja, Bw Ranguma alikubali kumuunga mkono Bw Obura. Seneta Outa pia alitangaza kuunga mkono mwafaka huo, hali iliyowafanya wawaniaji wengine kumuunga mkono Bw Obura kwa pamoja,” zikaeleza duru.

Ikizingatiwa Bw Obura anatoka katika eneo la Kano ambalo lina idadi kubwa ya wapigakura, mwafaka huo unaonekana kuwa mtihani mkubwa kwa Prof Nyong’o.

You can share this post!

Vita vya magavana, Kalonzo pigo kwa Raila Ukambani

Kingi amezewa ODM ikimkwaza

T L