• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:55 AM
Kenya Kwanza: Ruto asema ‘form’ ni kubembeleza vyama tanzu kukubali kuvunjwa vijiunge na UDA

Kenya Kwanza: Ruto asema ‘form’ ni kubembeleza vyama tanzu kukubali kuvunjwa vijiunge na UDA

NA CECIL ODONGO

RAIS William Ruto mnamo Ijumaa amepigia debe pendekezo la baadhi ya vyama tanzu ndani ya Kenya Kwanza kuvunjwa ndipo viungane na UDA kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 ila akasema havitalazimishwa.

Katibu Mkuu wa UDA Cleophas Malala amekuwa katika mstari wa mbele kupigia debe pendekezo kuwa vyama tanzu ndani UDA vivunjwe ili kuwe na chama kimoja dhabiti kuelekea kura hiyo.

Kati ya vyama ambavyo Bw Malala amekuwa akipigia upato vivunje ni Ford Kenya na ANC ambavyo vina  ufuasi mkubwa Magharibi mwa nchi. Ford Kenya inaongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi.

Bw Malala alinukuliwa akisema vyama hivyo ni vya vijiji na Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale ni kati ya wanasiasa ambao walikuwa wamemshutumu hadharani na kumtaja kama kiongozi anayezua mgawanyiko ndani ya Kenya Kwanza.

Uongozi wa Ford Kenya, ANC, PAA na vyama vingine tanzu umekuwa ukipinga kauli ya Bw Malala na kusisitiza kuwa havitajiunga na UDA. Hata hivyo, tayari vyama tisa ndani ya Kenya Kwanza vimekubali kuwa vitavunjwa na kujiunga na UDA vikiwemo UMP, FPK, EFP, CCM, NAP na Chama cha Kazi

“Nimeskia wengine wetu wakisema hawa wenzetu lazima wafanye hivi na vile, hapana. Unasema tu ni vizuri kama wangejiunga na sisi,” akasema Rais Ruto.

Alikuwa akiwahutubia wajumbe wa UDA katika Ukumbi wa Bomas wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho.

Alisema ni kupitia mazungumzo na maelewano ndipo vyama hivyo vinaweza kukubali hatimaye kujiunga na UDA.

“Tunaweza kuzungumza na kukubaliana ili wajiunge nasi ndipo tuwe na chama imara Kenya,” akaongeza.

Wakati wa mkutano huo, UDA ilitangaza kuwa uchaguzi wake wa mashinani utaandaliwa mnamo Disemba 9 mwaka huu na wanachama watatumia mfumo wa kidigitali kuwachagua viongozi wao.

  • Tags

You can share this post!

Napoli yamuomba radhi Osimhen baada ya kumkejeli alipokosa...

Jinsi mateka wa bangi alivyofyeka familia ya watu nane...

T L