• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:55 AM
Kesi ya Sonko na IEBC kuhusu idhini ya kuwania ni wiki ijayo

Kesi ya Sonko na IEBC kuhusu idhini ya kuwania ni wiki ijayo

NA PHILIP MUYANGA

OMBI la gavana wa zamani wa Nairobi, Bw Mike Sonko, la kupinga uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumzuia kuwania ugavana Mombasa, litasikilizwa Juni 14.

Hakimu John Mativo alieleza kuwa kesi hiyo itatoa mwelekeo iwapo uamuzi wa IEBC wa kumzuia Bw Sonko kuwania ugavana utasimamishwa kwa muda, kesi hiyo ikiendelea kusikilizwa.

Sonko alipewa siku tatu awasilishe hati za kesi hiyo kwa tume ya IEBC, kwa matayarisho ya kesi hiyo Jumanne ijayo.

Kufikia sasa, Mwenyekiti wa IEBC Bw Wafula Chebukati tayari alishateua kampuni ya sheria itakayowasilisha tume katika kesi hiyo inayofanyika Mahakama Kuu ya Mombasa.

Katika maombi ya Bw Sonko, anaitaka IEBC na Bw Chebukati kubatilisha uamuzi wa kumzuia kuwania ugavana.

Bw Chebukati alitoa uamuzi huo kupitia taarifa kwa vyombo vya habari mnamo Jumamosi iliyopita.

Gavana huyo wa zamani Nairobi pia ameitaka mahakama isuluhishe suala la afisa wa kusimamia uchaguzi katika Kaunti ya Mombasa, kukataa kumkubalia agombee kiti cha ugavana.

Kupitia kwa wakili wake Bw Derrick Odhiambo, Bw Sonko ameeleza kuwa kesi ya kubanduliwa kwake kama gavana wa Nairobi bado inaendelea katika Mahakama ya Juu.

Kwa hivyo, alihoji, uamuzi wa kumzuia kuwania ugavana Mombasa ni njia isiyo ya haki ambayo inalenga kumhujumu.

Alisema kuwa uamuzi huo umemuumiza na kumsababishia uharibifu mkubwa sana.

Bw Sonko ametaka kesi hiyo kusikilizwa haraka iwezekanavyo.

“Suala hili ni la muhimu sana kwa umma. Ni vyema haki itolewe kwangu haraka iwezekanavyo. Muda haupo nasi,” alisisitiza mlalamishi.

Kulingana na mwanasiasa huyo, tume ya IEBC ilimbagua kwani kuna wawaniaji wengine ambao walibanduliwa ofisini ama wana kesi katika Mahakama ya Rufaa, lakini walikubaliwa kugombea viti.

Anataka mahakama imlazimishe Bw Chebukati kupokea karatasi zake za uteuzi na kisha amuidhinishe kuwania ugavana Mombasa.

  • Tags

You can share this post!

Kithi, Mung’aro na Tinga wamenyana kwa mdahalo Kilifi

Austria ya kocha Ralf Rangnick yaendeleza masaibu ya...

T L