• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:55 AM
Kibarua kwa Samboja kiti chake kikimezewa mate

Kibarua kwa Samboja kiti chake kikimezewa mate

Na LUCY MKANYIKA

GAVANA wa Kaunti ya Taita Taveta, Bw Granton Samboja anakabiliwa na ushindani mkali anapotarajia kutetea kiti chake katika uchaguzi wa mwaka ujao.

Kufikia sasa, wanasiasa watano wametangaza nia ya kuwania kiti hicho. Wao ni mtangulizi wake John Mruttu, aliyekuwa seneta Dan Mwazo, Mbunge wa Mwatate Andrew Mwadime, mtaalamu wa masuala ya mawasiliano, Bi Patience Nyange na wakili Stephen Mwakesi.

Katika mahojiano na Taifa Leo, watano hao, walidai wananchi wanahitaji uongozi mpya ili kufanikisha maendeleo katika Kaunti hiyo.

“Kuna tatizo katika kaunti hii ambalo tawala mbili za kaunti hazijafanikiwa kutatua. Ni wakati wa kutafuta kiongozi mwingine,” akasema Bw Mwazo.

Mwanasiasa huyo alikuwa mbunge wa Voi mwaka wa 2007, kabla ya kuhudumu kama seneta wa kwanza wa Taita Taveta 2013.

Aliwania ugavana 2017 kupitia Chama cha Jubilee lakini akaibuka katika nafasi ya tatu.Bi Nyange ambaye ndiye mwanamke pekee katika kinyang’anyiro hicho kwa sasa, alisema anaamini ana uwezo wa kutosha kuongoza kaunti hiyo.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, aliyekuwa naibu mkuu wa Benki Kuu ya Kenya, Bi Jacinta Mwatela, aliwania wadhifa huo, lakini kufikia sasa hajatangaza kama atakuwa debeni.

Hata hivyo, Naibu Gavana Majala Mlaghui, alitetea utendakazi wa serikali ya kaunti akisema uongozi wa Bw Samboja umefanikisha miradi mingi ya maendeleo na imepanga kuendeleza mtindo huo katika kaunti nzima.

“Jukumu letu kuu ni kustawisha kaunti yetu. Kuna maliasili tele hapa ambazo zinaweza kuleta mabadiliko. Tutafanikiwa vipi ikiwa tutaendelea kubadilisha viongozi kila mara?” akauliza Bi Mlaghui.

Bw Mruttu ambaye alipoteza kiti hicho 2017, alisema lengo lake ni kuhakikisha kuwa miradi aliyoanzisha wakati alipokuwa gavana imekamilishwa.

“Hali si nzuri katika sekta za afya na kilimo. Kuna mengi ambayo yameharibika na yanahitaji kuboreshwa kwa sababu watu wetu wanateseka,” akasema.

Kulingana naye, mipango aliyoanzisha kama vile ununuzi wa trekta za kusaidia wakulima zimekwama kwa sababu zisizoeleweka.

Katika uchaguzi uliopita, alipata kura 21,596 huku Bw Samboja akishinda na kura 37,079.Kwa upande wake, Bw Mwadime ambaye amekuwa mbunge wa Mwatate tangu 2013, alisema ameshinikizwa na wito wa wakazi kuwania kiti cha ugavana.

“Awali sikuwa na uhakika lakini sasa nimeamua kuwania kiti hicho. Nimefanyia watu wa Mwatate mengi na niko tayari kutumikia kaunti nzima,” akasema.

Bw Mwakesi ambaye anatarajiwa kuwania kiti hicho kupitia United Democratic Alliance (UDA) ambacho kinahusishwa na Naibu Rais William Ruto, huenda akalazimika kupigania tikiti ya chama hicho na Bw Mruttu na Bw Mwazo kwani wote wameonekana kuegemea upande huo.

Aliyekuwa Mbunge wa Wundanyi, Bw Thomas Mwadeghu aliamua kubadili nia ya kuwania ugavana akatangaza atawania useneta.

Bw Mwadeghu aliwania ugavana kupitia ODM mwaka wa 2017 akaibuka wa nne baada ya Samboja, Mruttu na Mwazo.

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Walimu wakuu wanaoendelea kutoza ada za...

TAHARIRI: Saba Saba iende mbali, isirudi tena