• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: Saba Saba iende mbali, isirudi tena

TAHARIRI: Saba Saba iende mbali, isirudi tena

NA  MHARIRI

KENYA leo inatarajia kuadhimisha miaka 31 tangu vuguvugu la Saba Saba lilipoundwa.

Vuguvugu hilo ambalo liliundwa mnamo Julai 7, 1990, lilikuwa na lengo la kupinga utawala wa serikali unaodhulumu haki za raia humu nchini.

Tangu wakati huo wa utawala wa aliyekuwa rais Daniel arap Moi, taifa hili lilifanikiwa kupiga hatua kubwa katika masuala mbalimbali yaliyolenga kufanikisha uongozi bora.

Tofauti na ilivyokuwa katika miaka iliyotangulia, Kenya ilijiinua kidemokrasia na hatimaye kufanikiwa kupitisha katiba mpya mwaka wa 2010.

Katiba hiyo ilisifiwa kimataifa kwa kutoa kipaumbele kwa masuala ambayo yalikuwa yakitatiza nchi kwa miaka mingi kama vile ukosefu wa usawa katika ugavi wa rasilimali, uhuru wa vitengo muhimu vya kitaifa kama vile mahakama, bunge na idara ya polisi, miongoni mwa mengine.

Hata hivyo, kuna hofu kuwa mafanikio haya yote yameingia hatarini katika miaka michache iliyopita.

Hii ni kutokana na malalamishi mengi yanayohusu dhuluma zinazotendwa na polisi dhidi ya wananchi na viongozi wanaokosoa serikali, maamuzi yanayofanywa bungeni kwa njia inayoashiria kuwa kitengo hicho hakina uhuru, malalamishi ya majaji kuwa inakandamizwa na serikali iliyo mamlakani, na malalamishi sawa na hayo ya mahakama kutoka kwa vitengo vingine vya kitaifa vinavyostahili kuwa huru kikatiba kama vile Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kando na serikali kuu ambayo pia hulaumiwa kwa kushindwa kutumia vyema rasilimali za umma kwa manufaa ya wananchi, baadhi ya serikali za kaunti pia zimenyoshewa kidole cha lawama kwa kukosa kufanikisha maazimio ya wananchi kwa kuleta maendeleo waliyotarajia kupitia kwa mfumo wa ugatuzi.

Haya yote yanaashiria kuwa, kuna hatari ya kupoteza mafanikio yote yaliyopatikana kufikia sasa ikiwa taifa hili halitapata viongozi, kutoka wa mashinani hadi wa serikali kuu, ambao wanajali masilahi ya umma.

Ni wajibu wa raia kutumia mamlaka yao ya kikatiba kushinikiza viongozi waliopo wawe waadilifu na wenye maazimio yatakayoleta mafanikio kwa maisha ya umma badala ya kujitafutia makuu kibinafsi.

Bila hilo, tutazidi kushuhudia hali ambapo raia wataendelea kunyanyaswa kwa njia mbalimbali na vilio vinavyosikika sasa vitadumu kwa vizazi vijavyo.

You can share this post!

Kibarua kwa Samboja kiti chake kikimezewa mate

Uhuru sasa kuzuru Ukambani