• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kibicho atajwa katika masaibu ya Ngirici UDA

Kibicho atajwa katika masaibu ya Ngirici UDA

Na NICHOLAS KOMU

JINA la Katibu katika Wizara Usalama wa Ndani Karanja Kibicho limetajwa katika masaibu yanayomkumba Mbunge Mwakilishi wa Kirinyaga Wangui Ngirici ndani ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Inadaiwa kuwa Bi Ngirici ametengwa katika chama hicho kinachohusishwa na Naibu Rais William Ruto kutokana na ukuruba kati yake na Dkt Kibicho.

Katibu katika Wizara Usalama wa Ndani Karanja Kibicho akihutubu kwenye hafla ya awali. PICHA | MAKTABA

Katika siku za hivi karibuni, mbunge huyo mwakilishi wa Kirinyaga na mumewe, Andrew Ngirici, wameonekana pamoja na Kibicho katika hafla mbalimbali ishara kwamba wamezika tofauti baina yao.

Kumekuwa na uhasama mkubwa kati ya Bw na Bi Ngirici kwa upande mmoja na Dkt Kibicho kwa upande mwingine. Lakini hatua ya uamuzi wao wa kuzika uhasama huo mnamo Septemba mwaka huu ndio ulichangia masaibu ya Bi Ngirici katika UDA.

Watu wenye ushawishi ndani ya UDA waliambia Taifa Leo kwamba hatua ya mbunge huyo kusonga karibu na Dkt Kibicho ilitilia shaka uaminifu wake kwa Dkt Ruto.

Hii ni kwa sababu Naibu huyo wa Rais haelewani na Dkt Kibicho, ambaye anatoka kaunti ya Kirinyaga.

“Hatua ya Bi Ngirici kusongea karibu na Kibicho ilichangia uaminifu wake kutiliwa shaka. Tulitaka mtu mwaminifu kwa UDA katika kaunti ya Kirinyaga na Mlima Kenya kwa ujumla. Kwa ujio wa Gavana Waiguru ulionekana kujaza pengo hilo,” akasema mwana mikakati mmoja wa UDA.

Bi Ngirici pia amekuwa akishinikiza kwamba ateuliwe moja kwa moja kama mgombeaji ugavana kwa tiketi ya chama cha UDA, pendekezo ambalo limepingwa na Naibu Rais Dkt Ruto.

Gavana Waiguru anapania kutetea kiti chake katika uchaguzi mkuu ujao, kwa tiketi ya chama cha UDA.

Hii ina maana kuwa Bi Ngirici, ambaye ni mmoja wa mwanasiasa maarufu katika kaunti ya Kirinyaga, atalazimika kushiriki katika mchujo wa UDA au ahame chama hicho.

Gavana Waiguru sasa anaonekana kujaribu kujikita kama mshirika mkuu wa Dkt Ruto katika kaunti ya Kirinyaga. Kwa upande wake, Bi Ngirici hajatoa mwelekeo wake mpya wa kisiasa.

Lakini kuna dalili kwamba Bi Ngirici anapanga kuhama chama cha UDA.

Akiongea juzi katika shule ya msingi ya Kiamugumo, Bi Ngirici alisema atajikita katika ndoto yake ya kisiasa pekee wala sio masuala mengine.

Hii ni tofauti na msimamo wake wa hapo awali ambapo amekuwa akipigia debe azma ya urais ya Dkt Ruto ndani na nje ya kaunti ya Kirinyaga.

Akiwa katika mkutano huo aliwaambia wakazi wa Kirinyaga kwamba hataki kujua jinsi watakavyowachagua viongozi wengine mradi tu wampe kura za ugavana.

“Sina shida na yule ambaye mtampigia kura. Wale wanaotaka kumpigia kura Ruto waendelee; na wale ambao wanataka kumpigia kura Raila waendelee kufanya hivyo. Lakini naomba kura zenu kwa wadhifa wa Ugavana,” akaeleza.

Wafuasi wa Ngirici wanasema kuwa hatua ya Dkt Ruto kumkaribisha Bi Waiguru katika chama cha UDA, ilionyesha usaliti kwake (Ngirici) ikizingatiwa kuwa mbunge huyo ametumia muda na rasilimali zake nyingi kuvumisha chama cha UDA.

You can share this post!

Kithi akanusha madai anamezea ugavana

Viongozi waahidi kampeni za amani Rift Valley

T L