• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:30 PM
Kioni atabiri Kenya Kwanza itakufa 2027

Kioni atabiri Kenya Kwanza itakufa 2027

NA MWANGI MUIRURI

KATIBU Mkuu wa chama cha Jubilee, Bw Jeremiah Kioni, mnamo Jumanne alitabiri kuwa serikali ya Rais William Ruto itahudumu kwa muhula mmoja.

Aliilaumu kwa kuwa na kisasi na inayojumuisha “mtu mwenye kuharibu mambo” – Naibu Rais wake – “anayezunguka akiwasukuma watu kila mahali”.

Akizungumza katika runinga ya Citizen, Bw Kioni alisema “ haijalishi iwapo wanapanga kuiba uchaguzi mkuu wa 2027 au watakuwa na kaka na dada zao kama Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)… hawataona muhula wa pili”.

Bw Kioni aliongeza kuwa Bw Gachagua kwa kweli ni mtu mwaminifu anavyodai kila mara “na kwa kutekeleza uaminifu wake, amewafichulia kisasi kinachoendeshwa na serikali ya Rais Ruto”.

Alisema kukiri kwa Bw Gachagua kuwa alifanya baadhi ya makamishna wa maeneo kufutwa na wengine kusimamishwa kazi, wengine wengi kuhamishwa, alionyesha wazi kuwa wanaadhibu wale wanaochukuliwa kuwa marafiki wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta.

Jumapili, Bw Gachagua, akizungumza katika runinga ya Inooro alifichua kuwa “juzi nilikuwa Nyeri na nikaagiza Kamishna wa Eneo la Kati, Bi Esther Maina awakamate watengenezaji wote wa pombe haramu ndani ya siku tatu pamoja na wahudumu wa baa wahalifu na wauzaji wa mihadarati”.

Bw Gachagua alifichua kuwa “alidhani ni mzaha na leo ametimuliwa.. wale makamishna wa kaunti pia watahamishwa… ni juu yao kuamua ni wao au ni wahalifu wanaosimamia kaunti”.

Bw Kioni alisema hii inaonyesha wazi kuwa serikali ya Dkt Ruto imeanza vita na wale inaotaka kuadhibu.

“Malalamishi yale waliyokuwa nayo kwamba marafiki zao walikuwa wakidhulumiwa serikalini ni utawala huo wanaotekeleza dhidi ya wanaochukuliwa kuwa marafiki wa Jubilee. Ujumbe unaotolewa hapa ni kwamba kubadilika kwa serikali ni kuadhibu marafiki wa serikali inayoondoka,” alisema.

Aliongeza kuwa serikali imeamua “kuwaandama wanaoitwa watu wa Uhuru wanaoshukiwa kuendeleza biashara na serikali”.

Ingawa serikali imeacha mpango wake wa kuunda tume ya mahakama kuchunguza waliotumia serikali kwa maslahi yao, Bw Gachagua Jumapili alitangaza kuwa “tutatwaa kimya kimya na kwa siri mali yao waliyopata kwa njia haramu, tutafuta mikataba na biashara zao, hatutalipa madeni wanayodai na kuchunguza biashara zao zinazoendelea”.

Bw Kioni alimuonya Bw Gachagua kwamba “mdomo huo wako ni habari njema kwa Rais Ruto ambaye atakutumia kujimaliza mwenyewe kwa maneno unayotamka”.

Alidai kwamba Bw Gachagua anajimaliza kisiasa mbali na kutiwa kwenye mtego wa kuiachilia jamii ya Wakikuyu.

Mnamo Jumapili, Bw Gachagua alikiri kwamba “kuna wale wanaolalamika kwamba anazungumza sana. Ni mapenzi ya Mungu kwamba niwe mwaminifu na siko tayari kubadilika hivi karibuni… itabidi mnivumilie kwa sababu nitanyamaza wakati mambo yatakapoanza kuimarika na kunufaisha watu wetu”.

  • Tags

You can share this post!

Chuo cha kiufundi chajengwa mjini Ruiru

Polisi 4 rumande kwa jaribio la kuiba Sh2m

T L