• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 AM
Kiunjuri aonekana kuasi Ruto na kujiunga na ‘Baba’

Kiunjuri aonekana kuasi Ruto na kujiunga na ‘Baba’

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa zamani wa Kilimo Mwangi Kiunjuri ameonyesha dalili za kuunga mkono ndoto ya kiongozi wa ODM Raila Odinga ya kuingia Ikulu 2022, baada ya kusema wakazi wa Mlima Kenya wataunga mkono mgombea atakayefanikisha marekebisho ya Katiba.

Bw Kiunjiuri ambaye ni kiongozi wa chama cha The Service Party (TSP) Jumapili alisema wakazi wa eneo hilo wataunga mkono mgombeaji urais atakayefanikisha mageuzi ndani ya siku 100.

“Sisi kama watu wa Mlima Kenya tutaunga mkono mgombeaji atakayetuhakikishia kuwa ndani ya siku 100 ya utawala wake, Katiba itafanyiwa marekebisho ili tupate maeneobunge 11 zaidi tulizoahidi. Maeneobunge haya yatatuwezesha kupata uwakilishaji sawa na Sh53 bilioni zaidi za maendeleo,” akaeleza alipohudhuria mazishi katika kijiji cha Siakago, Mbeere Kaskazini, Kaunti ya Embu.

Bw Kiunjuri alisema kuwa eneo la Mlima Kenya linaunga mkono usawa wa uwakilishaji ulivyopendekezwa katika Mswada wa Marekebisho ya Katiba, 2022.

Mswada huo, maarufu kama BBI, uliharamishwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa baada ya kubainisha kubainika kuwa waandilizi wake hawakushirikisha umma katika utayarishaji wake.

Katika kampeni zake chini ya kauli mbiu ya Azimio la Umoja Bw Odinga ameahidi eneo la Mlima Kenya kwamba atafufua Mswada wa BBI ili kuiwezesha eneo bunge hilo kupata maeneo bunge zaidi.

“Tutarejesha Mswada wa BBI ili mpate maeneo bunge 11 zaidi na Sh53 bilioni ambayo mlipoteza baada ya mahakama kusitisha shughuli ya marekebisho ya Katiba. Ningependa kuhakikishia kuwa tutarudisha Reggea wapende wasipende,” Bw Odinga akasema mnamo Septemba 1, 2021 alipopeleka kampeni zake katika eneo la Limuru, kaunti ya Kiambu.

Kiongozi huyo wa ODM alisema Mswada wa BBI ulilenga kufanikisha kanuni ya Mtu Mmoja, Shilingi Moja, Kura Moja, ambayo imekuwa ikipigiwa upatu na viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya.

Kulingana na Mswada huo eneo pana la Mlima Kenya lingepata maeneo bunge 11 zaidi kati ya maeneo bunge 70 mapya ambaye yangebuniwa kote nchini.

Lakini Naibu Rais William Ruto ameshikilia kuwa Mswada wa BBI haukuwa na manufaa yoyote kwa Wakenya ila kubuni nafasi zaidi ya uongozi kwa manufaa ya viongozi wachache “walafi”.

Jumamosi, Bw Kiunjuri alionekana kutofautiana na kauli hii ya Dkt Ruto akiitaja kama uwongo na njama inayolenga kuwakosesha wakazi wa Mlima Kenya uwakilishi sawa pamoja na ugavi wa rasilimali.

“Hawatuambii manufaa ya BBI kwetu kama wakazi wa Mlima Kenya. Wanatuhadaa kuwa ni dhima ya mswada huo ni kubuni nafasi zaidi kwa viongozi wa kisiasa. Wanaweza kuonda pendekeza la kubuniwa kwa nyadhifa zaidi za uongozi lakini waache kanuni ya Mtu Mmoja, Shilingi Moja, Kura Moja,” a”asema Bw Kiunjuri, akionekana kurejelea suala la idadi zaidi za maeneo bunge.

Kulingana na Bw Kiunjuri, marekebisho ya Katiba yatawezesha eneo la Mlima Kenya kupata uwakilishi sawa na ugavi sawa wa rasilimali kutoka Serikali ya Kitaifa.

Hii ni kinyume na kampeni ambayo kiongozi huyo wa chama cha TSP alikuwa akiendeleza mwaka jana ambapo aliwaonya wakazi wa Mlima Kenya dhidi ya kuunda mkono ripoti ya BBI, hata kabla ya kutolewa kwake kwa umma.

“Eneo letu limekabiliwa na changamoto nyingi kwa sababu ya kuwa na idadi kubwa ya watu na uwakilishi finyu kwa sababu kiongozi wa taifa anatoka eneo letu. Mtu asiwadanganye kwamba wao ndio wenye usemi wa kisiasa katika eneo hili,” Bw Kiunjuri akawaambia waombolezaji.

Akaendelea, “Tutampigia kura mgombeaji ambaye atasuluhisha matatizo yetu kama vile uhaba wa maji, uwakilishi usio sawa miongoni mwa mengine. Yule ambaye atatuhakikishia kuwa kura yetu ina thamani.”

Bw Odinga amekuwa akiwahakikishia wakazi wa Mlima Kenya kuwa licha ya mahakama kuzima mpango wa kuidhinisha mapendekezo ya mswada wa BBI kupitia kura ya maamuzi, mchakato huo utaendelea baada yake kuingia Ikulu.

Kwa kuunga mkono mchakato wa marekebisho ya Katiba, Bw Kiunjuri sasa anaonekana kujihusisha na msimamo wa mrengo wa Bw Odinga na kujitenga na ule wa Dkt Ruto.

Hii ni licha ya kwamba Mbunge huyo wa zamani wa Laikipia Mashariki amekuwa mfuasi sugu wa vuguvugu wa hasla huku akipigania nafasi ya kuwa mgombea mwenza wa Naibu Rais katika kinyang’anyiro cha urais.

Bw Kiunjuri ameonekana kupoteza matumaini ya kutwaa nafasi hiyo baada ya Dkt Ruto kusisitiza kuwa sharti avunje chama chake cha TSP na kujiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Dkt Ruto ametaja TSC, Chama cha Kazi (CCK) kinachoongozwa na Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, kama vyama vya kikabila. Hii ni licha ya vyama hivyo kuunga mkono azma yake ya kuingia Ikulu 2022.

Hii ndio maana Mbw Kiunjuri na Kuria wameungana na kiongozi wa Narc- Kenya Martha Karua kubuni muungano wa Umoja wa Mlima Kenya. Walisema wanapania kupigania masilahi ya eneo la Mlima Kenya chini ya mwavuli wa muungano huo.

You can share this post!

Walioathirika kutokana na kero ya nzige wanaendelea kupata...

Presha kwa Solskjaer miti ya Man-Utd ikizidi kuteleza

T L