• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Kumbe wana doa!

Kumbe wana doa!

NA WANDERI KAMAU

HATUA ya wawaniaji wanne wa urais walioidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutoa ahadi za kila aina kwa Wakenya imeibua maswali ikiwa wamegeuka ‘malaika’ wapya ghafla, ikizingatiwa kuwa matendo yao ya awali ni ya kutiliwa shaka.

Vigogo hao ni Naibu Rais William Ruto, Raila Odinga (Azimio-One Kenya), Prof George Wajackoyah (Roots Party of Kenya) na Bw Mwaure Waihiga (Agano Party of Kenya).

Licha ya kutoa msururu wa ahadi za kuboresha maisha ya Wakenya ikiwa atachaguliwa rais Agosti, Dkt Ruto anakabiliwa na tuhuma za kushiriki katika maovu tofauti ya kijamii ambayo yanatilia shaka ufaafu wake.

Naibu kiongozi wa nchi aliwahi kushtakiwa kwa kunyakua ardhi ya mkazi mmoja wa Eldoret, Bw Adrian Muteshi, sakata ya uuzaji mahindi katika serikali ya Mzee Mwai Kibaki, sakata ya ‘Ndege ya Hustler’, unyakuzi ardhi inayomilikiwa na Shule ya Msingi ya Lang’ata (Nairobi) kati ya maovu mengine.

Kwenye suala la Bw Muteshi, Dkt Ruto alishtakiwa mahakamani na kupatikana na hatia. Katika kesi hiyo, Bw Muteshi alikuwa amemshtaki Dkt Ruto kwa kumnyang’anya ardhi yake yenye ukubwa wa ekari 100 eneo la Bonde la Ufa wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Bw Muteshi pia alisema baada ya kunyakua ardhi hiyo, Dkt Ruto alimfukuza pamoja na wafanyakazi wake.

Lakini akitoa uamuzi huo mnamo Juni 2013, Jaji Rose Ougo wa Mahakama Kuu ya Nairobi, alimwagiza Dkt Ruto kuondoka mara moja kwenye ardhi hiyo na kumlipa fidia ya Sh5 milioni.

Sakata ya mahindi iliibuka 2009, wakati Dkt Ruto alikuwa akihudumu kama Waziri wa Kilimo.

Kampuni ya Pricewaterhouse Coopers ilifanya ukaguzi, ambapo ilibainika kuwa, Dkt Rito alimtumia msaidizi wake wa kibinafsi kuiandikia barua Halmashauri ya Kitaifa ya Kununua Nafaka (NCPB) kumtengea rafikiye magunia 1,000 ya mahindi.

Dkt Ruto alinusurika kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye Bungeni, baada ya Spika Kenneth Marende kukataa stakabadhi zilizowasilishwa zikimhusisha na sakata hiyo.

Sakata ya Ndege ya ‘Hustler’ ilitokea mnamo 2013, mwezi mmoja baada ya serikali ya Jubilee kuchukua hatamu za uongozi. Mnamo 2013, Dkt Ruto alituhumiwa kukodisha ndege ya kibinafsi kwa gharama ya Sh100 milioni kwa ziara katika eneo la Afrika Magharibi. Ziara hiyo ilikuwa ya kuyarai mataifa ya eneo hilo kuiunga mkono Kenya kwenye kesi iliyomkabili pamoja na Rais Uhuru Kenyatta katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Ziara hiyo iliwagharimu walipaushuru jumla ya Sh21 milioni.

Hata hivyo, baada ya kuchunguza suala hilo, Kamati ya Uhasibu ya Bunge (PAC) iliwalaumu maafisa wakuu wa serikali ya Jubilee kwa kukiuka taratibu za utoaji zabuni. Ripoti pia ilimlaumu Rais Kenyatta kwa kutotoa maagizo kwa Dkt Ruto kwa njia ifaayo.

Kwa upande wake, Bw Odinga amekuwa akihusishwa na sakata kadhaa, baadhi zikihusisha unyakuzi Kiwanda cha Kutengeneza Sukari Nguru (Mollases) cha Kisumu, uporaji wa fedha za mpango wa Kazi Kwa Vijana (KKV) alipohudumu kama Waziri Mkuu katika serikali ya Bw Kibaki kati ya vingine.

Hata hivyo, Bw Odinga amekuwa akijitetea dhidi ya unyakuzi wa kiwanda hicho, akisisitiza kuwa alikipata kwa njia halali.

Kwa upande mwingine, licha ya ahadi zake nyingi, Prof Wajackoyah analaumiwa kwa kuwa miongoni mwa watu walioendesha mateso dhidi ya watu walioikosoa serikali ya marehemu Daniel Moi katika Vyumba vya Mateso vya Nyayo.

Lakini kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni majuzi, Wajackoyah alisema yeye alikuwa miongoni mwa watu waliolengwa na utawala huo, ndipo akatafuta hifadhi ya kisiasa nchini Uingereza na baadaye nchini Amerika.

Kulingana na Bw Javas Bigambo, ni wazi Wakenya wanawachagua viongozi wale wale ambao wamewapora nyakati za hapo awali.

“Wakenya wanapaswa kujilaumu wenyewe kwa kukubali hadaa za viongozi ambao wamekuwa siasani kwa muda mrefu bila kuleta mageuzi hata kidogo. Ni kinaya kuwa wengi wanaamini utakuwa mwanzo mpya chini ya vigogo hao,” akaeleza.

Kauli kama hiyo ilitolewa na mchanganuzi Mark Bichachi, aliyesema kuwa, Wakenya hawafai kufanya maamuzi ya kisiasa kulingana na mawimbi ya kisiasa yaliyopo.

Bw Mwaure Waihiga naye anakosolewa kwa kuwa “kibaraka wa watu kutoka juu” kuwania urais, ili kuvuruga karata za kisiasa katika uchaguzi huo.

Wakosoaji wake wanamtaja kuwa “mradi wa kisiasa”, wakisema hana umaarufu wa kisiasa ikilinganishwa na vigogo wengine.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Rais alishindwa kabisa kukabili jinamizi...

DOMO: Eti Zari Hassan kavimba kichwa!

T L