• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 8:50 AM
Kutana na seneta wa Lamu ambaye ndiye mwanasiasa kipenzi cha wazee

Kutana na seneta wa Lamu ambaye ndiye mwanasiasa kipenzi cha wazee

NA KALUME KAZUNGU

‘PALIPO wazee hapaharibiki neno’ ndiyo msemo na kauli mbiu ya Seneta wa Lamu Joseph Githuku Kamau, ambaye mapenzi yake kwa wazee yanazidi kumzolea sifa kochokocho ndani na nje ya Kaunti ya Lamu.

Mara nyingi akiwa eneo lake la Lamu, iwe ni kisiwa cha Faza, Amu, Matondoni, Kiunga, Kizingitini, Pate, Mtangawanda, Ndau, Siyu, Hindi, Mokowe, Mpeketoni, Witu na kwingineko, utampata seneta Githuku akiwa amekaa au kusimama ilhali amezingirwa na kadamnasi ya wazee wakimpa wosia kwa upendo huku wakiangua vicheko.

Mara nyingine pia utampata seneta Githuku, akiwa amekaa kitako mabarazani na wazee waliokula chumvi nyingi, wakibugia kahawa chungu na kupiga gumzo kwa furaha, dhihirisho tosha kwamba kiongozi huyo ni mwenye fahari kuu kwa mababu hao.

Taifa Jumapili ilichimba chini kutaka kujua ni nini hasa chanzo cha seneta Githuku kuwa na ukaribu zaidi na wazee licha ya ujana wake?

Katika mahojiano ya kipekee na Bw Githuku, seneta huyo alifichua wazi kwamba yeye binafsi kabla na hata baada ya kujitosa siasani na uongozini, kitovu chake cha ushauri au mawaidha ni hao wazee.

Seneta wa Lamu Joseph Githuku Kamau. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kulingana na Bw Githuku, ushirikiano wake na wazee umemwezesha kusimama tisti kwenye ulingo wa siasa, akitaja kuwa wazee wameona mengi na kwamba wako na tajiriba ya maisha ambayo katu haipatikani darasani au kwenye mfumo au mtaala wowote wa elimu ya sasa.

Anasema yeye hutegemea sana wazee kumwelekeza katika uongozi wake, hivyo kufaulu si haba.

“Waswahili walituambia kuishi kwingi ndiko kuona mengi. Hivyo hawa wazee siwezi kuwadharau, kuwabagua au kuwatenga katika uongozi wangu. Mimi ni kijana tu na ni bayana mengi ya maisha siyafahamu. Na hii ndiyo sababu nikaamua kwamba mimi na wazee na wazee na mimi. Wao hunielekeza ni wapi pa kwenda, ni lipi nifanye na la kuepuka. Nitakuwa nikikaa chini ya ushauri wa hawa wazee ambao kweli wameona mengi. Hiyo ndiyo siri inayonifanya mimi kukita mizizi siasani na kuongoza vyema jamii yangu ya Lamu na Jamhuri ya Kenya kwa ujumla,” akasema Bw Githuku.

Aliwashauri viongozi wenza, hasa wale ambao bado ni limbukeni siasani, kuwa na hulka ya kuenzi mawaidha ya wazee, akisisitiza kuwa ni hao hao wazee ambao ndio wenye ukwasi wa ufahamu zaidi wa jamii husika kuliko mtu yeyote yule.

“Kila ninapokanyaga maeneo haya ya kaunti ya Lamu huwa na kibaraza changu maalum cha wazee. Nikienda Faza, najua nitapatana na wazee fulani. Nikienda Kizingitini, najua nitawapata wazee kama vile Yusuf Omar Athman ama Ahmed Swalehe Bwanamkuu na wengineo. Nikikaa chini kupokea wosia wa hawa wazee niko na imani kubwa kwamba siwezi kupotea kamwe kiuongozi,” akasema Bw Githuku.

Baadhi ya wazee waliohojiwa na Taifa Jumapili hawakuficha furaha yao kuhusiana na mapenzi yao kwa seneta Githuku.

Mzee Yusuf Omar Athman,70, mkazi wa kisiwa cha Kizingitini, alimtaja seneta Githuku kuwa kiongozi mchapa kazi, mwadilifu na ambaye hana ubaguzi na jamii ya Lamu ambayo imejumuisha karibu makabila yote zaidi ya 42 ya Kenya.

Bw Athman pia alimtaja seneta Githuku kuwa karimu kwa watu wake anaowaongoza, hali ambayo imewafanya kumpenda kiongozi huyo hata zaidi.

“Yeye ni mpenda amani. Hachagui wala kubagua kabila unalotoka. Kinyume na maseneta wengine watangulizi wake waliokuwa wakibagua baadhi ya maeneo, hasa Lamu Mashariki na kukosa kuyatembelea baada ya kuchaguliwa, seneta Githuku yeye amekuwa akitembelea kila sehemu mara kwa mara kukutana na watu wake. Tunamuombea azidi kudumu kitini,” akasema Bw Athman.

Naye Ahmed Swalehe Bwanamkuu,67, mkazi wa Lamu Mashariki, alisema moyo safi wa seneta Githuku wa kutaka kuisaidia jamii yake anayoiongoza umewaondolea wazazi mzigo wa kugharimia chakula cha wanafunzi shuleni.

Seneta wa Lamu Joseph Githuku Kamau (kulia) akizungumza na wazee katika kisiwa cha Faza, Lamu Mashariki mnamo Septemba 13, 2023. Seneta huyo tangu alipoingia mamlakani amekuwa kipenzi cha wazee, akisema yeye hutumia wazee kumwelekeza katika uongozi wake. PICHA | KALUME KAZUNGU

Ni kupitia shinikizo mara kwa mara za seneta Githuku kwa serikali kuu, ambapo wanafunzi wa shule za msingi, kuanzia chekechea hadi darasa la nane kote Lamu wanafurahia mpango wa lishe shuleni.

Bw Bwanamkuu alisema wazazi wengi, hasa wale wa kutoka jamii zisizojiweza kwa sasa wameondolewa msongo wa mawazo kuhusiana na jinsi watoto wao wanafaa kukaa shuleni kusoma.

“Hatusumbukii tena ni nini watoto wetu watakula shuleni au watasoma vipi. Wale wa chekechea hasa wanakunywa uji asubuhi ilhali mchana wanakula mchele na maharagwe. Haya yote ni kutokana na bidi za seneta wetu Githuku za kuiosukuma serikali kuu kutekeleza mpango huo. Na ndiyo sababu tunampenda huyu seneta Githuku kama wakazi wa Lamu, hasa sisi wazee. Ni kiongoza mwema,” akasema Bw Bwanamkuu.

Bi Mary Wanjiku, mkazi wa tarafa ya Mpeketoni, alisema upendo wake kwa seneta Githuku unatokana na kigezo kwamba yeye amewapa kipaumbele wazee, hasa katika kutetea maslahi yao serikalini.

“Wazee wote wa miaka 70 kuendelea wafaa kupokea fedha za kila mwezi kutoka serikali kuu. Twamshukuru seneta Githuku kwani amekuwa akisukuma sisi wazee tusajiliwe na kupokea kiinua mgongo kutoka kwa serikali kuu kila mwezi. Viongozi wengine wamekuwa wakikwepa kabisa suala hili la kututetea sisi wazee kimaslahi isipokuwa seneta Githuku,” akasema Bi Wanjiku.

Wazee hao aidha waliwashauri viongozi wengine wa kaunti ya Lamu kuiga mfano wa seneta Githuku kwa kuhakikisha wanazuru sehemu zote za Lamu, kutangamana na wananchi wa tabaka zote, iwe ni maskini au tajiri, wazee au vijana, akina baba au akina mama hata watoto.

Bw Githuku alichaguliwa kwa mara ya kwanza kama seneta wa kaunti ya Lamu kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022, akiwabwaga wapinzani wake saba kwenye kinyang’anyiro hicho kwa kujizolea kura 12,091.

Alichaguliwa kupitia tiketi ya chama cha Jubilee kilichoko kwenye mrengo wa Azimio La Umoja-One Kenya Alliance.

Ikumbukwe kuwa Bw Githuku pia amewahi kuhudumu kama diwani maalum wa Bunge la Kaunti ya Lamu kati ya mwaka 2013 na 2017, akiteuliwa kupitia chama cha Farmers Party.

  • Tags

You can share this post!

BAHARI YA MAPENZI: Raha ya ndoa ni ‘kusumbuliwa’

Wa Iria ‘amshambulia’ Gavana Kahiga kwa kumfinyia jicho

T L