• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
BAHARI YA MAPENZI: Raha ya ndoa ni ‘kusumbuliwa’

BAHARI YA MAPENZI: Raha ya ndoa ni ‘kusumbuliwa’

NA BENSON MATHEKA

KUNA watu wasiopenda kupigiwa simu kila wakati na waume au wake wao.

Wanahisi kwamba kufanya hivyo ni kuwasumbua na kuwachunga na hivyo kuwanyima uhuru wao.

Ugomvi umekuwa ukizuka mume au mke akiuliza kwa nini mwenziwe hajibu simu zake au mmoja akilalamikia mwenzake kwa kumsumbua kwa simu na jumbe kila wakati.

Hata hivyo, japo kila mtu ana haki ya kuelezea mwenzake hulka zinazomsinya, na simu za kila mara zinaweza kuudhi, ukweli wa mambo ni kuwa mawasiliano ni muhimu kwa ufanisi wa ndoa.

Hivyo basi, watu hawafai kuwachukulia waume au wake wao kuwa wasumbufu iwapo wanachofanya ni kujenga uhusiano wao.

Wasichofahamu wanaolalamika ni kuwa mapenzi hujengwa kupitia usumbufu.

Iwapo mume au mke hakusumbui kwa chochote, iwe ni kutafuta ushauri wako, kukuomba usaidizi au kukuhitaji uwe karibu naye, basi ana kasoro. Usumbufu unaochosha baina ya wanandoa ni ule unaovuka mipaka au wa kutaka yasiyowezekana kwa nguvu au kutumia mwingine vibaya.

Tabia ya mtu ikivuka mipaka, inaweza kukosesha mtu amani na huo ni usumbufu mbaya. Katika uhusiano wowote wa ndoa, madai ya usumbufu huibuka mawasiliano yakipungua au kukosekana. Kupigiana simu sio usumbufu na kuchoshwa na tabia ya mume au mkeo ya kutaka kuzungumza nawe kunaweza kumfanya atilie shaka uaminifu wake kwako.

Mruhusu mtu wako awe na uhuru wa kuwasiliana nawe. Usimfanye akuogope au kumsukuma ahisi kana kwamba haumpendi. Mchumba anayemsumbua mwenzake akitaka kuwa karibu naye anajenga uhusiano wao.

Lakini iwapo unahisi mtu wako anakusumbua akiwa au akitaka kuwa karibu nawe, uhusiano wenu una dosari inayofaa kurekebishwa kwa haraka na hakuna njia nyingine isipokuwa kuimarisha mawasiliano.

Maisha ya ndoa ni kusaidiana na mchumba anayehisi mwenzake anasumbua kwa matakwa yake, huwa ana mapenzi ya dhati.

Hata hivyo, ni lazima matakwa hayo yawe anayoweza kutimiza mume au mke. Unapoingia katika ndoa, kuwa tayari kusumbuliwa. Hii ni kwa sababu huwa umetoa maisha yako kwa mtu mwingine na kuhisi anakusumbua ni kumaanisha haujampatia maisha yako kikamilifu. Usumbufu mbaya katika ndoa ni dhuluma pekee.

Ningetaka watu watofautishe kati ya usumbufu na mateso. Pia, ni vizuri kufahamu kinachomvutia au kumsinya mtu wako ili ukitumie au kukiepuka katika uhusiano wenu.

Nasisitiza kuwa uhusiano wa mapenzi usiokuwa na usumbufu chanya huwa haujakamilika. Ikiwa uko na mchumba na hakusumbui kwa chochote ikiwemo kutaka umtimizie haki zake za ndoa, basi chunguza uhusiano wenu.

Ndoa inafanya wawili kuwa kitu kimoja na kwa hivyo mtu hafai kuhisi mwenzake anamsumbua mradi tu sio dhuluma na unyanyasaji. Kilele cha raha ya ndoa ni wakati mtu anaposumbuliwa na mwenzake akitaka burudani na hali huwa kinyume mtu anayesumbuliwa.

  • Tags

You can share this post!

Wachuuzi wanavyohatarisha maisha yao Nairobi-Nakuru Highway

Kutana na seneta wa Lamu ambaye ndiye mwanasiasa kipenzi...

T L